WHO inasema fedha hizo zinahitajika kushughulikia milipuko ya ghafla pamoja na migogoro ya muda mrefu ya kibinadamu, ambapo mifumo ya afya iko chini ya shinikizo kubwa.Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus, amesema wito huo ni zaidi ya misaada ya kawaida. “Huu si msaada wa hisani . Ni uwekezaji wa kimkakati katika afya na usalama, unaorejesha utu, kuimarisha jamii na kufungua njia ya kujikwamua.”
Gari la Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), ambalo linasimamia usafirishaji wa wagonjwa hadi kuvuka mpaka wa Rafah siku ya kwanza ya kufunguliwa tena.
Kivuko cha Rafah
Mashariki ya Kati, wakati muda ukiendelea kuyoyoma kwa maelfu ya wagonjwa mahututi huko Gaza, kufunguliwa tena kwa kivuko cha Rafah kunaleta mwanga wa matumaini.
Kivuko hicho kilifunguliwa Jumatatu baada ya kufungwa kwa zaidi ya mwaka mmoja, chini ya mpango wa amani unaoungwa mkono na Marekani, na kuruhusu uhamisho wa kwanza wa wagonjwa tangu mwaka 2025.
Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa Duniani, WHO, linasema wagonjwa watano pamoja na wasindikizaji wao saba wamehamishwa salama leo kwenda Misri kwa msaada wa Umoja wa Mataifa. Hata hivyo, mahitaji bado ni makubwa.
“Tumeweza kuwahamisha wagonjwa watano, jambo ambalo ni la kutia moyo,” amesema msemaji wa WHO, Christian Lindmeierakiongeza kuwa “lakini kwa hakika tunahitaji kuwahamisha wengi zaidi.”
Zaidi ya wagonjwa 18,500 bado wanahitaji huduma maalum za matibabu ambazo hazipatikani ndani ya Ukanda wa Gaza.
Midoli ya watoto ikiwa imefunikwa na barafu nje ya nyumba huko Kyiv wakati wa kukatika kwa umeme kwa majira ya baridi kali nchini Ukraine.
Msimu wa baridi nchini Ukraine
Na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia watoto UNICEF leo liimesema linaongeza juhudi zake za msaada wa msimu wa baridi nchini Ukraine huku watoto na familia wakikabiliwa na kukatika kwa umeme, kukosa vipasha joto na maji kufuatia mashambulizi yanayoendelea dhidi ya miundombinu ya nishati na baridi kali.
Tangu Novemba, shirika hilo limesambaza jenereta 106 kote nchini kusaidia huduma za maji na mifumo ya kupasha joto, huku takribani jenereta 150 zaidi zikitarajiwa kuwasili katika wiki zijazo.
Msaada huo, unaoungwa mkono na serikali za Uingereza, Marekani na Denmark, unalenga kuhakikisha hospitali, shule na makazi vinaendelea kufanya kazi wakati wa kukatika kwa huduma.