
Dar es Salaam. Mwimbaji mkongwe na mtunzi wa muziki wa taarabu nchini, Ally Hemed ‘Ally Star’ amefariki dunia leo, Februari 3, 2026 katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili alikokuwa amelazwa.
Ally Star ambaye amefanya kazi kwa muda mrefu akiwa na bendi ya Tanzania One Theatre (TOT), alikuwa amelazwa Muhimbili kwa takriban wiki tano.
Akizungumza na Mwananchi, Mkurugenzi wa T.O.T, Khadija Kopa amesema Ally Star amefariki dunia akiwa anapambania afya yake katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
“Ni kweli huzuni sana Ally Star amefariki leo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, alikuwa amelazwa kwa muda akiwa anapatiwa matibabu, taratibu za mazishi tutawajuza baada ya muda kidogo,” amesema Khadija Kopa.
Enzi za uhai wake Ally Star aliimba nyimbo maarufu kama Zumbukuku, Limbukeni, Natanga na Njia, Hauvumi Lakini Umo na nyingine nyingi.
Katika uhai wake, Ally Star aliwahi pia kuzitumikia bendi kama Muungano Cultural Troupe, Orchestra King Kikii Double O na Bima Modern Taarab.