Mnamo Februari 2022, FIFA na UEFA zilitangaza kuiwekea Urusi na vilabu vyake marufuku ya kushiriki mashindano yoyote ya kimataifa “hadi taarifa zaidi,” baada ya uvamizi wake nchini Ukraine.
Hatua hiyo ilimaanisha kutengwa kwa timu ya taifa, vilabu vya Urusi, pamoja na kuondolewa kwenye fursa za kushiriki michuano mikubwa kama Kombe la Dunia la FIFA na Ligi ya Mabingwa barani Ulaya.
“Marufuku hii haijafanya lolote, imesababisha tu kuchanganyikiwa na chuki zaidi,” Infantino aliiambia Sky Sports.
Aliongeza kuwa kuruhusu vijana wa Urusi kushiriki michezo katika maeneo mengine ya Ulaya “kungeweza kusaidia” kupunguza mvutano.
Infantino alisema FIFA “haipaswi kamwe kuifungia nchi yoyote isicheze mpira kwa sababu ya matendo ya viongozi wao wa kisiasa,” akisisitiza umuhimu wa kuendeleza mawasiliano ya kimichezo.
Kauli ya Infantino yakosolewa na Ukraine
Waziri wa Michezo wa Ukraine, Matvii Bidnyi, alikosoa vikali matamshi hayo, akiyaeleza kuwa “yasiyowajibika” na “yasiyoakisi uhalisia.”
“Zinatenganisha kandanda na ukweli kwamba watoto wanauawa,” Bidnyi aliambia Sky Sports.
Kwa upande mwingine, Rais wa UEFA, Aleksander Ceferin, ameendelea kushikilia msimamo kwamba vita nchini Ukraine lazima vikome kabla ya Urusi kurejeshwa katika mashindano, akirejea matamshi aliyoyatoa katika mkutano wa kufunga wa Bunge la UEFA Aprili mwaka jana.
Infantino pia alitetea uamuzi wa FIFA kumpa Rais wa Marekani, Donald Trump, tuzo ya amani wakati wa upangaji wa makundi ya Kombe la Dunia 2026.
“Chochote tunachoweza kufanya ili kusaidia amani duniani, tunapaswa kukifanya. Tumekuwa tukitafakari kwa muda mrefu kuhusu jinsi ya kuwatunuku wale wanaochangia katika amani,” alisema Infantino.
“Bila kuegemea upande wowote, Trump anastahili.”