Kuelekea siku ya kuelimisha umma kuhusu saratani Februari 04, shirika la Umoja wa Mataifa la Afya duniani, WHO linaendelea na harakati zake za kusaidia nchi wanachama kutokomeza saratani ya shingo ya kizazi ifikapo mwaka 2030 kupitia mikakati mbali mbali ikiwemo ya kusogeza huduma maeneo ya ndani na kuhakikisha huduma zinatolewa sambamba na huduma nyingine za afya.
Uzinduzi wa Mpango wa Kitaifa wa Kutokomeza Saratani ya Shingo ya Kizazi nchini Kenya 2026–2030.
Hatua ya hivi karibuni ni nchini Kenya ambapo taifa hilo la Afrika Mashariki limezindua Mkakati wa Kitaifa wa kutokomeza saratani ya shingo ya kizazi ifikapo mwaka 2030.
Dkt. Joseph Mogga, Afisa wa WHO nchini Kenya alipohojiwa na Assumpta Massoi wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa hakumung’unya maneno kuhusu hatua hiyo ya Kenya akisema ni tukio la kihistoria na limefanyika wakati muafaka.
“Saratani ya shingo ya kizazi ni miongoni mwa sababu kuu za vifo vinavyotokana na saratani nchini Kenya. Inaathiri sana vibaya watu, hasa wanawake. Kulingana na ripoti ya Wizara ya Afya ya Kenya, mwaka 2024, takribani wanawake 6,000 waligunduliwa kuwa na saratani ya shingo ya kizazi. Kati yao, wanawake 3,600 walifariki dunia,” amesema Dkt.Mogga.
Ameongeza kuwa, hiyo ni sawa na takribani wanawake 10 hufariki kila siku. Ni idadi kubwa sana ya wanawake wanaokufa, kwa kuwa unaweza kufikiria wanawake 10 wakifariki kila siku kutokana na saratani ya shingo ya kizazi.
Amesema Mkakati huo pamoja na mambo mengine unaotoa mwelekeo wa jinsi ya kuzuia, kugundua mapema na kutibu wanawake.
Bado jamii haielewi kuwa saratani ya shingo ya kizazi ina kinga na tiba
Alipoulizwa kulikoni saratani ya shingo ya kizazi inaua wanawake 10 kila siku nchini Kenya, ilhali ina kinga na tiba, Dkt, Mogga amesema changamoto ni uelewa hasa maeneo ya vijijini.
Amesema, “wanawake hawafahamu kwamba saratani ya shingo ya kizazi inaweza kuzuilika. Pia hawajui kwamba saratani ya shingo ya kizazi inaweza kugunduliwa mapema na kutibika. Sehemu kubwa ya tatizo hili pia inatokana na ukweli kwamba huduma hazipatikani kwa urahisi katika maeneo ya karibu nao, hasa vijijini. Huduma za uchunguzi zipo, na huduma za matibabu zipo, lakini wanawake hulazimika wakati mwingine kutembea umbali mrefu hadi kufika vituo vikuu au vituo vya afya ambako huduma hizi kwa kawaida hupatikana. Kwa hiyo, uzinduzi wa mpango huu ni muhimu sana kwa sababu unashughulikia changamoto nyingi zinazokabiliwa kwa sasa.”
Mpango wa 90-70-90 ni nini?
Je ni nini tafsiri ya mpango wa Kenya kutokomeza saratani ya shingo ya kizazi kwa kuzingatia 90-70-90? Dkt. Mogga amefafanua akisema “Katika mkakati huu, lengo kuu ni kuhakikisha kwamba asilimia 90 ya wasichana wanalindwa dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi kupitia chanjo kabla ya kufikisha umri wa miaka 15. Asilimia 70 ya wanawake wanapimwa kwa vipimo vyenye ufanisi wa hali ya juu angalau mara mbili katika maisha yao, na kisha asilimia 90 ya wale wanaobainika kuwa na matokeo yasiyo ya kawaida wanapatiwa matibabu.”
Kuboresha upatikanaji wa uchunguzi na matunzo ya saratani ya matiti na mlango wa kizazi kupitia mradi wa Huduma za Saratani za Wanawake (WICS) katika kaunti za Nyandarua na Bungoma, Kenya.
Hivyo amesema kuwa mkakati huu unajikita katika kinga, uchunguzi wa mapema na matibabu, pamoja na kuhakikisha kuna muunganiko mzuri wa huduma za afya. Ukitekelezwa kikamilifu, unaweza kusababisha kutokomeza kabisa saratani ya shingo ya kizazi, kama ambavyo tumeona katika baadhi ya nchi kama Australia, ambayo huenda ikawa miongoni mwa nchi za kwanza kabisa kutokomeza saratani ya shingo ya kizazi kutokana na utekelezaji wa mkakati huu.
Sasa watoto wa kike wanapatiwa dozi moja tu ya Human Papiloma Virus (HPV)
WHO imepongeza sana Wizara ya Afya ya Kenya kwa kuanza kutumia chanjo ya dozi moja. Dkt. Mogga anasema, “haya ni mabadiliko ya kihistoria, kwa sababu awali chanjo ilikuwa inatolewa kwa dozi mbili kwa tofauti ya miezi sita, na wasichana wengi walikuwa hawarejei kwa dozi ya pili. Kwanza kabisa, sasa hutolewa dozi moja ambayo imethibitishwa kuwa na ufanisi mkubwa. Pili, changamoto zinazohusiana na ufuatiliaji zimekuwa tatizo kubwa, hasa katika maeneo ya vijijini. Hivyo basi, mfumo huu ni rahisi kutekelezwa, ni wa gharama nafuu na una ufanisi sawa. Kwa hiyo, mabadiliko haya yamekuwa muhimu sana kwa Kenya na huenda pia kwa ukanda mzima.”
Mradi wa WICS ni jawabu mujarabu kusaidia kukabili saratani ya shingo ya kizazi
Tayari WHO imesaidia Kenya kuanzisha na kutekeleza Mradi wa Huduma Jumuishi za saratani kwa wanawake, WICS katika kaunti za Nyandarua na Bungoma, hatua ambayo Dkt. Mogga anasema, “Mradi huu unalenga kujumuisha huduma za uchunguzi wa wanawake katika huduma za kawaida za afya, hasa huduma za msingi zilizo karibu na jamii wanamoishi watu. Hivyo, mwanamke anapokuja hospitalini—iwe ni kwa ajili ya ushauri wa malaria, huduma za kliniki ya wajawazito, au huduma nyingine zozote za kawaida—pia hupimwa katika mazingira hayo hayo, akihudumiwa na mhudumu yuleyule wa afya. Uchunguzi huu unahusisha saratani ya shingo ya kizazi pamoja na magonjwa mengine yasiyoambukiza kama kisukari na shinikizo la damu.”
Kuboresha upatikanaji wa uchunguzi na matunzo ya saratani ya matiti na mlango wa kizazi kupitia mradi wa Huduma za Saratani za Wanawake (WICS) katika kaunti za Nyandarua na Bungoma, Kenya.
Wahamasishaji wa afya wa kijamii nao wanajumuishwa
Kwa mujibu wa Afisa huyo wa WHO nchini Kenya, “sehemu nyingine muhimu sana ya mradi huu ni kushirikiana na wahamasishaji wa afya ngazi ya jamii. Huduma zinaunganishwa ndani ya mfumo wa wahamasishaji wa afya ya jamii, ambapo wahamasishaji hao hutembelea jamii, kutoa elimu vijijini na kuhamasisha huduma hizi. Hivyo, watu wanapokuja hospitalini huwa tayari wanafahamu kwamba wanaweza kupimwa, na hata wakikosa fursa hiyo wanaweza kuomba huduma. Kwa sasa tunaona kwamba mradi wa WICS unafanya kazi vizuri, ikiwa ni pamoja na kushirikiana na serikali za kaunti ili kuhakikisha umiliki wa mradi. Viongozi na wahudumu pia wanapewa elimu na mafunzo wakati wa utekelezaji wa mradi huu. Kwa hiyo, tunasema kwamba huu labda ni moja ya njia bora zaidi za kufanyia uchunguzi wanawake.”
WHO ina matumaini Kenya itatokomeza saratani ya shingo ya kizazi ifikapo 2030
Dkt. Mogga anasema wana matumaini kwamba Kenya itatokomeza kwani tayari imeonesha dhamiri kubwa ya kisiasa. Mosi kwa kuzindua Mkakati wa kutokomeza; Pili kwa kujitolea kuwapatia bure wasichana chanjo ya HPV. “ Chanjo zinapokuwa bure, kinachobaki ni kuangalia jinsi ya kuwahamasisha wasichana kupata chanjo, kwa kuwa ni bure kabisa—hakuna hata shilingi moja ya Kenya inayolipwa kwa ajili ya chanjo.Hii ni dhamira thabiti sana ya kisiasa kutoka kwa Kenya, pamoja na utayari wa kuunganisha huduma za afya katika ngazi ya huduma za msingi.
Halikadhalika kwa kuanzishwa kwa Mfuko wa Huduma za Msingi za Afya ambao unafadhiliwa na serikali ya kitaifa, inamaanisha kuwa huduma zitakuwa bure katika ngazi ya huduma za msingi.Haya yote ni maamuzi makubwa na ya kishujaa kutoka kwa serikali, ambayo sisi kama washirika tunayachukulia kama hatua muhimu sana, na tunaamini kwa hakika kuwa nchi inaweza kufikia malengo yaliyowekwa,” ametamatisha Dkt. Mogga.