Serikali imewahakikishia wananchi wa Jiji la Mbeya kuwa utekelezaji wa mradi mkubwa wa maji kutoka chanzo cha Mto Kiwira unaendelea na unatarajiwa kukamilika mwezi Disemba 2026, hatua itakayomaliza changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama katika eneo hilo.
Akijibu swali leo Februari 3 Bungeni, jijini Dodoma Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Kundo Mathew, amesema Serikali inaendelea kutekeleza mradi wa kusafirisha maji kutoka Mto Kiwira kwenda Jijini Mbeya kama sehemu ya mkakati wa kuboresha huduma ya maji kwa wakazi wa jiji hilo na maeneo ya jirani.
Ameeleza kuwa kazi zinazoendelea kutekelezwa kupitia mradi huo ni pamoja na ujenzi wa dakio (intake) na mtambo wa kisasa wa kutibu maji wenye uwezo wa kuzalisha lita milioni 117 kwa siku.
Aidha, mradi huo pia unahusisha ujenzi wa matanki mawili ya kuhifadhi maji yenye uwezo wa kuhifadhi lita milioni 10 kila moja, sambamba na ulazaji wa mabomba ya kusafirisha maji kwa umbali wa kilometa 37.
Naibu Waziri ameongeza kuwa utekelezaji wa mradi huo hadi sasa umefikia wastani wa asilimia 48, hali inayoonesha hatua nzuri ya maendeleo ya kazi licha ya changamoto mbalimbali.
Swali kuhusu utekelezaji wa mradi huo liliulizwa Bungeni na Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini, Mheshimiwa Patrick Adkin Mwalunenge, ambapo mradi huo unatarajiwa kunufaisha zaidi ya wakazi 890,000 wa Jiji la Mbeya na Mji wa Mbalizi pindi utakapokamilika.
(Feed generated with FetchRSS)