Rais wa Marekani Donald Trump anasema India imekubali kuacha kununua mafuta ghafi kutoka Urusi. Makubaliano hayo yanatarajiwa kusababisha Marekani kupunguza ushuru wake wa forodha wa ziada kwa bidhaa za India kutoka asilimia 50 hadi asilimia 18.
Trump alisema katika mitandao ya kijamii Februari 2 kwamba Waziri Mkuu wa India Narendra Modi alikubali kununua mafuta ghafi zaidi “kutoka Marekani na, pengine, Venezuela.”
Rais huyo wa Marekani aliongeza kuwa India “itapiga hatua mbele” ili kupunguza ushuru wa forodha na vikwazo vingine visivyo vya ushuru wa forodha dhidi ya bidhaa za Marekani. Pia alisema Modi imejitolea kununua bidhaa za Marekani, ikiwa ni pamoja na bidhaa za nishati na kilimo, zenye thamani ya zaidi ya dola bilioni 500.
Modi aliandika kwenye mitandao ya kijamii Februari 2, “Shukrani kubwa kwa Rais Trump kwa niaba ya watu bilioni 1.4 wa India.” Lakini hakuzungumzia mpango wowote wa kuacha kununua mafuta ghafi kutoka Urusi.
India imeendelea kuagiza mafuta ghafi kutoka Urusi bila kujiunga na Marekani na mataifa mengine ya Magharibi katika kuweka vikwazo dhidi ya nchi hiyo. India imekuwa katika nafasi ya pili katika ununuzi mkubwa zaidi wa mafuta kutoka Urusi baada ya China.
Agosti mwaka jana, utawala wa Marekani uliongeza ushuru wa forodha wa jumla dhidi ya India hadi asilimia 50, ukitaja ununuzi wa mafuta ghafi na bidhaa za petroli kutoka Urusi kama sababu.