Ripoti katika vyombo vya habari vya kimataifa zimeashiria kwamba baada ya mazungumzo na viongozi wa jumuiya ya kijeshi ya NATO, Rais wa Marekani Donald Trump anafikiria kuweka vituo vya kijeshi vya Marekani kwenye kisiwa cha Greenland kama vile vya Uingereza katika kisiwa cha Cyrpus. 

Ripoti hizo za vyombo vya habari zinakumbusha makubaliano ya kipekee yaliyofikiwa kati ya Uingereza na Cyprus tangu mwaka wa 1960, wakati nchi hiyo ilipopata uhuru kutoka Uingereza.

Cyprus ilitawaliwa na Uingereza kwa miongo kadhaa na ilipata uhuru wake mnamo mwaka 1960 baada ya mapambano ya mtutu wa bunduki.

Ingawa tangazo la uhuru mnamo mwaka 1960, liliashiria mwisho rasmi wa utawala wa kikoloni wa Uingereza, kisiwani Cyprus, halikumaanisha Uingereza kujiondoa kabisa kutoka kisiwani humo. Mkataba uliofikiwa ulitoa nafasi kwa Uingereza kuendelea kuyakalia maeneo mawili ya  Cyprus. Maeneo hayo ambayo ni vituo vya kijeshi vya Uingereza ni Akrotiri na Dhekelia.

Greenland 2026 | Maandamano ya kuipinga hatua ya Trump
Maandamano yazuka kisiwani Greenland kuhusu mpango wa Trump kuelekea kisiwa hicho Picha: Marko Djurica/REUTERS

Vituo hivyo kwa pamoja vipo katika eneo la kilometa 254 za mraba sawa na takriban asilimia 3 ya ukubwa wa Cyprus. Na kwa mujibu wa makubaliano Uingereza hailipi chochote kwa matumizi  wa vituo hivyo. Badala yake Uingereza ilipaswa kutoa msaada wa fedha kwa Cyprus. 

Hata hivyo kisiwa cha Cyprus kiliupata msaada huo kwa muda wa miaka mitano tu baada ya Uingereza kuusimamisha msaada huo mnamo mwaka 1965 kwa madai kwamba mazingira yalibadilika kutokana na mgogoro uliozuka kwenye kisiwa hicho.

Baada ya karibu mwongo mmoja wa mapigano, kisiwa cha Cyprus kiligawanywa katika sehemu mbili. Moja ni jumuiya ya watu wenye nasaba ya kigiriki na nyingine ni ile ya watu wenye nasaba ya kituruki. Palifanyika jaribio la kuipindua serikali lilioungwa mkono na Ugiriki lakini Uturuki iliingilia kati kijeshi mnamo mwaka 1974.

Upande unaoitwa Jamhuri ya Cyprus wenye watu wenye nasaba ya kigiriki ni mwanachama wa Umoja wa Ulaya. Na ule upande mwingine wa Cyprus wa watu wenye nasaba ya kituruki hautambuliwi na jumuiya ya kimataifa. Je, nani anavidhibiti vituo vya kijeshi vya Uingereza nchini Cyprus? 

Vituo hivyo, Akrotiri na Dhekelia bado vinadhibitiwa kikamilifu na Uingereza miaka 65 baada ya Cyprus  kuanza kujitawala. Maeneo hayo mawili yapo chini ya mamlaka ya wizara ya ulinzi ya Uingereza. Hadhi ya maeneo hayo haikubadilika baada ya Cyprus kujiunga na Umoja wa Ulaya mnamo mwaka 2004.

Je, Cyprus ina usemi wowote kuhusu vituo hivyo vya kijeshi?

Mkataba wa kujiunga na Umoja wa Ulaya uliweka itifaki iliyoruhusu kuyaweka maeneo hayo mawili ya Cyprus nje ya sheria za Umoja wa Ulaya.

Ingawa shughuli za kijeshi za Uingereza kwenye vituo hivyo vya Akrotiri na Dhekelia zinafanyika kwa njia ya faragha, vyombo vya habari vya Uingereza vimeripoti juu ya kuhusika kwa vikosi vya Uingereza na vya washirika wa NATO katika operesheni za kijeshi zinazohusiana na Iraq, Syria, Yemen na Gaza.

Mnamo mwaka 2024 msemaji wa serikali ya Cyprus alitoa tamko baada ya kufanyika maandamano ya kupinga vituo hivyo kutumika kwa ajili ya migogoro ya Mashariki ya Kati. Hata hivyo kwa mujibu wa mkataba uliofikiwa, Uingereza  haiwajibiki kutoa taarifa yoyote kwa  serikali ya Cyprus juu shughuli za kijeshi  kwenye vituo hivyo.

Hata hivyo mwito juu ya kufungwa kwa vituo hivyo si wa sauti kubwa, miongoni mwa vyama vya kisiasa kisiwani Cyprus. Aliyekuwa mwanasheria mkuu wa Jamhuri wa Cyprus amesema uwepo wa vituo hivyo vya kijeshi chini ya mamlaka Uingereza ni kukiuka sheria za kimataifa. Mwanasheria huyo amesema huo ni mwendelezo  wa ukoloni.

Naye Kostas Paraskevas, profesa wa Sheria ya Umma na Haki za Binadamu ambaye pia ni rais wa Idara ya Sheria katika Chuo Kikuu cha Cyprus, ameiambia DW kwamba uhuru juu ya kambi za kijeshi za Uingereza sio kamili, kwani chini ya Mkataba wa Kuanzishwa kwa kambi hizo, Uingereza ilichukua majukumu maalum na ya wazi ya kutoendesha baadhi ya vitendo katika kambi hizo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *