Kwa mujibu wa Shirika la habari la Ukraine Ukrinform, milipuko kadhaa imesikika katika mji mkuu wa Kiev usiku wa kuamkia leo huku taarifa ambazo bado hazijathibitishwa zikisema kwamba mitambo miwili ya kuzalisha umeme wa joto ilishambuliwa. Baadae pia kulikuwa na ripoti za kushambuliwa makazi ya raia katika mji mkuu wa Kiev na kuwajeruhi watu wawili.

Maafisa wanasema mashambulizi hayo ya Urusi mjini Kiev yamesababisha zaidi ya majengo elfu moja ya makazi jijini Kyiv kukosa huduma ya umeme kwa ajili ya kupasha joto, huku baridi ikiwa kali chini ya nyuzi joto 20.

Mji wa mashariki mwa Ukraine wa Kharkiv, pia ulishambuliwa kwa makombora mawili, sambamba na ndege za kivita zisizo na rubani. Mashambulizi ya Urusi ya Droni pia yameripotiwa katika maeneo ya Zaporizhzhia na Dnipro na kumuua mwanamke mmoja.

Ukraine Kyiv 2026 | Wakaazi wakiwa wamejihifadhi kituo cha treni kufuatia mashambulizi ya Urusi mjini Kyiv
Wakaazi wakiwa wamejihifadhi kituo cha treni kufuatia mashambulizi ya Urusi mjini KyivPicha: Alina Smutko/REUTERS

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky, amesema Urusi imechagua kuendeleza mashambulizi zaidi kuliko mazungumzo ya amani, kufuatia mkururo wa mashambulizi ya usiku kucha. Amesema kwamba kitendo cha “kutumia siku za baridi kali zaidi kuwatia watu hofu ni muhimu zaidi kwa Urusi kuliko kugeukia diplomasia,” akiongeza kuwa vikosi vya Urusi vimefanya mashambulizi kwa kutumia  makombora yapatayo 70 na Droni karibu 450.

Urusi imekuwa ikipigana vita dhidi ya Ukraine kwa takriban miaka minne. Katika kipindi hiki, jeshi la Urusi limeharibu kwa mpangilio mitambo ya kuzalisha umeme na vituo vya kusambaza umeme.

Wiki iliyopita, Rais wa Marekani Donald Trump alisema kuwa Rais wa Urusi Vladimir Putin alikuwa amekubali, kwa ombi lake, kusitisha mashambulizi dhidi ya miundombinu ya nishati nchini Ukraine. Moscow hapo awali ilithibitisha hilo, lakini hata hivyo, mashambulizi ya hivi karibuni yanaashiria kuwa usitishwaji huo wa muda huenda umemalizika.

Wakati hayo yakiendelea mwanadiplomasia wa Uingereza katika Umoja wa Mataifa James Kariuki amesema London inaiunga mkono Ukraine katika mazungumzgo ya kusaka amani yanaoendelea. Kariuki ameongeza kwa kusema kwamba “Uingereza imejitolea kuharakisha msaada wake kwa Ukraine na kuweka shinikizo kubwa zaidi la kiuchumi kwa Urusi ili iweze kukaa meza ya kwa mazungumzo”, pamoja na washirika wake wa kimataifa,”

Ukraine Kyiv 2026 | Wakaazi wakiwa wamejihifadhi kituo cha treni kufuatia mashambulizi ya Urusi mjini Kyiv
Wakaazi wakiwa wamejihifadhi kituo cha treni kufuatia mashambulizi ya Urusi mjini KyivPicha: Alina Smutko/REUTERS

“Ukraine imeonyesha kuwa iko upande wa amani, huku Urusi ikiendelea kuzuia mchakato na kuitisha Ukraine pamoja na wananchi wake. Tunalaani mashambulizi mapya na ya kikatili ya Urusi dhidi ya miundombinu muhimu ya nishati na ya kiraia huko Kiev na maeneo mengine ya Ukraine, ambayo yameziacha familia zikikabiliwa na baridi kali na kunyimwa mahitaji ya msingi katikati ya majira ya baridi.”

Hapo jana Moscow ilithibitisha kwamba duru ya pili ya mazungumzo ya kusaka amani kati yake na Ukraine na Marekani, itafanyika Jumatano na Alhamis wiki hii huko mjini Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu. Rais Zelensky alidokeza siku ya Jumapili kwamba duru ijayo ya mazungumzo ya pande tatu itafanyika mapema wiki hii huko UAE.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *