
Utafiti wa kuaminika uliochapishwa na gazeti la Uingereza la The Guardian umehitimisha kwamba idadi ya watu wa Ukanda wa Gaza imepungua kwa takriban watu 254,000, au 10.6%, ikilinganishwa na makadirio ya kabla ya kuanza kwa vita vya mauaji ya kimbari ya Israel, Oktoba 7, 2023.
Utafiti wa kina uliofanywa na Chuo cha Sheria za Kimataifa za Kibinadamu na Haki za Binadamu cha Geneva umeripoti kwamba watoto 18,592 na takriban wanawake 12,400 waliuawa katika mashambulizi ya jeshi la Israel huko Gaza kufikia mwisho wa 2025.
Utafiti huo umeeleza kuwa licha ya makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyofikiwa Oktoba 2025, mamia ya Wapalestina wameuawa tangu wakati huo.
Utafiti huo umesema kwamba sheria ya kimataifa, ambayo inalenga kupunguza athari za vita, imefikia hatua ya kusambaratika huku uhalifu wa kivita ukishindwa kudhibitiwa, na wahalifu wakikwepa mkono wa sheria.
Karibu Wapalestina elfu 72 wameuawa shahidi tangu kuanza kwa vita huko Gaza, na zaidi ya wengine 171,000 wamejeruhiwa. Maelfu ya Wapalestina pia hawajulikani waliko na inaaminika kuwa bado wako chini ya vifusi vya majengo yaliyohariwa kwa mashambulizi ya Israel.
Ofisi ya Vyombo vya Habari ya Serikali ya Ghaza imesema zaidi ya Wapalestina 500 wameuliwa shahidi na jeshi la utawala wa kizayuni tangu usitishaji mapigano uliosimamiwa na Marekani huko Gaza ulipoanza kutekelezwa Oktoba 10.
Siku chache zilizopita pia, jeshi la utawala vamizi wa Israel lilikiri kwa mara ya kwanza – baada ya zaidi ya miaka miwili ya kukana mara kwa mara – usahihi wa data iliyochapishwa na Wizara ya Afya huko Gaza kwamba mashine ya mauaji ya Israel imeua Wapalestina zaidi ya 70,000 tangu Oktoba 7, 2023.
Inaripotiwa kwamba Israel iliangusha zaidi ya tani 200,000 za mada za milipuko wakati wa vita vyake dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza, kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na mamlaka rasmi huko Gaza.