Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa Ulimwenguni WHO limeelezea hatua hii kuwa muhimu, ingawa ni ndogo, wakati hali ya kibinadamu bado ni mbaya kwenye Ukanda wa Gaza.
Uhamisho wa kwanza wa wagonjwa tangu 2025
Msemaji wa WHO Christian Lindmeier akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva Uswis hii leo amethibitisha kuwa shirika la afya la Umoja wa Mataifa, pamoja na washirika wake, liliwezesha wagonjwa watano na wasindikizaji wao saba kuhamishwa kwenda Misri.
Lindmeier amesema “Huu ni uhamisho wa kwanza wa matibabu kupitia njia hii tangu mwaka wa 2025. Jukumu la WHO linalenga kuhakikisha usalama wa wagonjwa kutoka Gaza hadi mpaka wa upande wa pili Misri.”
Kivuko hicho cha mpakani kimefunguliwa kama sehemu ya mpango wa amani unaoungwa mkono na Marekani uliowasilishwa mnamo Septemba 2025.
Maelfu ya wagonjwa bado wanasubiri
Licha ya maendeleo haya madogo, WHO imetahadharisha kuwa idadi kubwa ya wagonjwa bado wamelazimika kubaki ndani ya Gaza, ambapo zaidi ya wagonjwa 18,500 bado wanahitaji matibabu maalum ambayo hayawezi kupatikana eneo hilo.
Lindmeier ameongeza kuwa “Tumeweza kuwahamisha watano, jambo ambalo ni zuri sana, lakini kwa hakika tunahitaji wengi zaidi. 18,500 wakiendelea kusubiri, watano tu wameweza kuondoka. Wengi wamebaki nyuma. Hii si hesabu tu ni janga la kibinadamu kwa wale walio na subira ya kusubiri.”
Wagonjwa waliohamishwa walichaguliwa na mamlaka ya afya ya eneo hilo, ambayo hutoa orodha ya kipaumbele kwa maafisa wa usalama. Mara tu ruhusa inapotolewa, WHO huandaa uhamisho na kuwajulisha familia.
WHOinasimamia mchakato wa wagonjwa wanaosafiri kwenda Misri kupata matibabu
Hali mbaya ya matibabu na mahitaji ya dharura
Msemaji wa WHO ameelezea hali mbaya ya wagonjwa walio Gaza, ikiwa ni pamoja na majeraha mabaya ya vita, saratani, kisukari, na magonjwa mengine sugu ambayo matibabu yake hayapatikani eneo hilo.
“Ni jambo baya sana unapoona msaada ukiwa pale kilomita chache tu nje ya mpaka, lakini haupatikani kwa sababu za kisiasa,” amesema Lindmeier, akionesha huzuni ya wagonjwa waliokufa wakiendelea kusubiri uhamisho wa matibabu.
Kabla ya mgogoro, mamia ya wagonjwa waliondoka Gaza kila siku kupitia Rafah kupata matibabu nje ya nchi. Lindmeier amesisitiza uhitaji wa dharura wa kurudisha mtiririko huu wa uhamisho.
“Tunahitaji kurudi kwenye hali hiyo,” amesema. “Tungetaka nchi nyingi zaidi ziwe tayari kusaidia. Hawa wagonjwa ndio wenye mahitaji makubwa, wenye hali za matibabu ambazo hakuna msaada ndani ya Gaza.”
Matarajio ya baadaye
WHO imeelezea uhamisho wa Jumatatu kama “jaribio” na hatua ya mwanzo kuelekea kuanzisha mchakato endelevu wa uhamisho wa matibabu, ukitoa tumaini dogo kwa maelfu ya wagonjwa walioko Gaza wakiendelea kusubiri.
“Sote tunaamini hii imefanikiwa hadi sasa,” Lindmeier amesema. “Lakini tunahitaji nchi nyingi zaidi ziwe tayari kusaidia.”