Witkoff, ambaye alihusika pakubwa kwenye kile kiitwacho “Mpango wa Amani wa Trump kwa Gaza” alitazamiwa kuwasili mjini Tel Aviv siku ya Jumanne (Februari 3), wakati kivuuko cha Rafah kwenye mpaka wa Misri na Ukanda wa Gaza kikifunguliwa jioni ya Jumatatu, hatua muhimu kwenye mpango huo ambayo ilishaakhirishwa mara kadhaa na utawala wa Israel. 

Hata hivyo, ni watu na bidhaa chache tu zilizoruhusiwa kuvuuka, huku maafisa wakisema ni watu 50 pekee walioweza kupita kutoka kila upande kwenda mwengine, kati ya Wapalestina wapatao 20,000 – watu wazima na watoto – wanaohitaji huduma ya haraka ya matibabu kuokowa maisha yao. 

Witkoff alipangiwa kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu katika mkutano utakaohudhuriwa pia na waziri wake wa ulinzi, Israel Katz, mkuu wa majeshi, Eyal Zamir, na mkurugenzi wa shirika la ujasusi la Mossad, David Barrea.

Zamil na Barrea walikuwa ziarani hivi karibuni jijini Washington.

Mazungumzo na Iran

Mkutano huo ulitazamiwa kufanyika wakati Wittkof akitarajiwa pia kuelekea Istanbul baadaye wiki hii kwa mazungumzo na wawakilishi wa Iran kusaka makubaliano juu ya mpango wa nyuklia wa Tehran, ambao unapingwa vikali na Israel na washirika wake. 

Steve Witkoff na Abbas Araghchi
Mjumbe Maalum wa Rais wa Marekani, Steve Witkoff (kushoto), anatazamiwa kukutana na Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Iran, Abbas Araghchi, nchini Uturuki.Picha: ERIC TSCHAEN/SISPA/picture alliance / SIPA | Vahid Salemi/AP/dpa/picture alliance

Netanyahu, ambaye amekuwa akiishinikiza Marekani kuishambulia Iran, anadai kuwa utawala wa Jamhuri hiyo ya Kiislamu ni hatari kwa uhai wa taifa la Israel, huku serikali mjini Tehran ikimuelezea waziri mkuu huyo wa Israel kama kikwazo kwa amani ya kweli ndani ya eneo zima la Mashariki ya Kati na Ghuba ya Uajemi. 

Siku ya Jumatatu (Februari 2) Rais Masoud Pezeshkian wa Iran aliamuru kufanyika kwa mkutano huo kutuliza taharuki iliyozuka tangu pale Rais Donald Trump wa Marekani alipotangaza nia ya kuivamia kijeshi Iran, kwa kisingizio cha kuwalinda waandamanaji waliokuwa wakipinga utawala baada ya maelfu kuuawa kwenye machafuko ya Disemba.

Abbas Araghchi, Iran
Ujumbe wa wapatanishi wa Iran kwenye mazungumzo ya kimataifa ukiongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje, Abbas Araghchi (katikati).Picha: Iranian Foreign Minister Abbas Araghchi Telegram messaging app/AP/dpa/picture-alliance

Hata hivyo, kwa siku za karibuni, Trump ameonekana kubadilisha kauli juu ya azma ya kuivamia Iran kutoka ile ya maandamano kurudi kwenye mpango wake wa nyuklia, miezi sita baada ya kutangaza kuuangamiza mpango huo kufuatia mashambulizi ya jeshi la Marekani dhidi ya vinu vya nyuklia vya Iran, yaliyotanguliwa na vita vya siku 12 vilivyoanzishwa na Tel Aviv dhidi ya Tehran.

Vyombo vya habari vya Iran na Marekani viliripoti kwamba Washington na Tehran wanapanga kurejea kwenye meza ya mazungumzo hivi karibuni, lakini vyombo vya habari nchini Israel vimeripoti kuwa maafisa wa ngazi za juu nchini humo wanatazamia kuwa mazungumzo yoyote kati ya pande hizo mbili yataishia kwenye mkwamo, na kwa hivyo kuuimarisha uwezekano wa mashambulizi ya Marekani dhidi ya Iran.

Hata hivyo, Iran imesema mara kadhaa kwamba mashambulizi yoyote dhidi yake yatajibiwa vikali na kwamba Israel na Marekani zitawajibika kwa chochote kitakachojiri. 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *