Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy anasema Urusi imehama kutoka kushambulia miundombinu ya nishati hadi “kuharibu” njia za usafiri, hasa reli, katika siku chache zilizopita.
Zelenskyy alisema hayo katika mitandao ya kijamii Februari 2. Aliongeza kuwa kazi ya kurejesha vituo vya nishati itaharakishwa kwani nyumba nyingi hazina vipashajoto kutokana na mashambulizi ya Urusi.
Ukraine inakabiliwa na ukosefu mkubwa wa umeme huku kukiwa na baridi kali. Mji mkuu, Kyiv, unatarajia halijoto ya juu zaidi ya nyuzi joto 11 hasi za Selisiasi wakati wa mchana hadi Februari 4. Vyombo vya habari vya nchi hiyo vinasema kwamba siku nne za kwanza za mwezi Februari huenda zikawa baridi zaidi katika kipindi cha miaka 20.
Mkazi wa Kyiv mwenye umri wa miaka 40 alisema umeme unapatikana kiasi kwa muda wa saa mbili kwa siku, na kupata umeme kwa saa nne inaonekana kama likizo. Alisema kwamba jiko la gesi ndicho chanzo pekee cha joto kwa familia yake, kwa hivyo kila mtu hukusanyika karibu nalo.