
Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za makao makuu ya chama cha ACT-Wazalendo zilizoko Vuga, mjini Unguja, Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Ismail Jussa amesema kwamba hatua ya kuazimia kuteketeza nyaraka za uchaguzi mkuu wa 2025 ina maana kwamba tume ya ZEC inakusudia kuharibu maendeleo ya kesi 25 zilizofunguliwa na wagombea waliopitishwa na chama hicho kuwania viti vya uwakilishi.
”ZEC imeamua kujificha chini ya kifungu cha 98 (3) cha Sheria ya Uchaguzi namba 4 ya mwaka 2018 kinachohusu kutunza nyaraka kwa siku 90. Tuweke wazi, ni kosa la jinai kuharibu ushahidi wakati kuna shauri la kisheria linaloendelea.”
Akinukuliwa na chombo cha habari cha serikali, Mkuu wa Divisheni ya Huduma za Sheria wa ZEC Ame Mohammed amesema tume hiyo iko tayari kutekeleza matakwa ya kisheria yanayoruhusu kuteketeza nyaraka za uchaguzi baada ya siku 90 tangu kumalizika kwa uchaguzi. Matamshi hayo aliyatoa jana katika waraka wake kwa waandishi wa habari.
”Kesi zipo mhakamani, lakini kesi zile hazihusiani na nyaraka kwa sababu hakuna zuwio la mahakama ambalo limeitaka tume kutotekeleza zoezi hili. Kwa hivyo zile kesi zipo, lakini mahakamani haijatoa zuwio na tume inatekeleza baada ya siku 90.” alisema Ame.
Wachambuzi wakosoa mpango wa kuchoma nyaraka za uchaguzi
Mchambuzi wa masuala ya kisiasa, Mohammed Salum amesema ZEC haipaswi kufanya haraka katika kuteketeza nyaraka na vielelezo vilivyotumika katika uchaguzi mkuu wa Zanzibar wa mwaka 2025.
Amesema ”Tume ya Uchaguzi kwa hili la kuteketeza nyaraka hatuoni umuhimu wake kwa kuwa wao ni mmoja wa watuhumiwa, hatuoni umuhimu wake nyaraka ni muhimu kwa kuwa zitahitajika kutumiwa mahakamani na vile vile huko nyuma hatujawahi kusikia kama nyaraka zimewahi kuteketezwa.”
Katika hatua nyengine chama cha ACT-Wazalendo kimetoa mapendekezo matatu ikiwemo ZEC kusitisha mara moja mpango huo hadi mashauri yaliopo mahakamani yamalizike, Mrajis wa mahakama kuu kushughulikia maombi ya chama hicho na ukaguzi wa nyaraka hizo, na kuzitaka mamlaka za ulinzi na usalama kuhakikisha kuwa nyaraka zote zinatunzwa chini ya ulinzi madhubuti ili kuzuwia moto wa ajali au upotevu.