London, England. Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta, amesema kufuzu kwa timu yake kwenye fainali ya Kombe la EFL (Carabao) ni matokeo ya kazi na subira ya miaka mingi, baada ya kuiondoa Chelsea kwa ushindi wa bao 1-0 katika mechi ya marudiano ya nusu fainali iliyochezwa jana Jumanne usiku.

Arsenal walikuwa tayari na faida ya ushindi wa mabao 3-2 walioupata Stamford Bridge, hivyo ushindi huo wa jumla ya mabao 4-2 umewapa tiketi ya kwenda kucheza mchezo wa fainali utakaopigwa kwenye Uwanja wa Wembley, Machi 22, 2026.

Mchezo wa marudiano ulikuwa wa tahadhari kwa pande zote mbili, huku nafasi za wazi zikiwa chache. Bao pekee la mchezo lilipatikana dakika za majeruhi kupitia shambulizi la kushtukiza, baada ya Declan Rice kumpasia Kai Havertz ambaye alimzidi ujanja kipa wa Chelsea, Robert Sanchez kabla ya kuupiga mpira wavuni.

Mshambuliaji wa Arsenal, Kai Havertz, wakati akifunga bao pekee dakika za majeruhi, katika ushindi wa 1-0 ilioupata Arsenal dhidi ya Chelsea kwenye mechi ya nusu fainali ya Kombe la Carabao jana Jumanne, Februari 3, 2026. Picha na Mtandao

Ushindi huo uliendeleza uimara wa safu ya ulinzi ya Arsenal, ambao sasa wameweka rekodi ya clean sheets 20 katika mashindano yote msimu huu, idadi ambayo wamewahi kuizidi mara moja tu chini ya Arteta msimu wa 2023-24 walipofanya hivyo mara 23.

Akizungumza baada ya mchezo, Arteta amesema amefurahia ushindi huo, hasa kutokana na ugumu wa mechi. “Tulijua itakuwa ngumu sana. Tulionyesha uimara na uzoefu wa mchezo tuliopaswa kuucheza.

Mazingira ya uwanja wetu yalikuwa maalum na yamechangia sana. Tumekuwa tukisubiri kwa miaka kadhaa kufika hatua hii, na sasa tumefanikiwa,” amesema Arteta.

Kiungo wa Arsenal, Declan Rice , akishangilia ushindi wa timu yake mara baada ya kutinga fainali ya Kombe la Carabao. Picha na Mtandao

Kwa upande wake, Declan Rice ameipongeza Chelsea kwa upinzani mkali walioutoa chini ya kocha wao mpya, Liam Rosenior.

Rice amesema ulinzi wa Arsenal ulikuwa imara na kusisitiza kuwa kikosi hicho kina njaa ya mafanikio.

“Tumekuwa karibu kwa misimu mitatu au minne iliyopita lakini hatukufanikiwa. Ndiyo maana msimu huu tuna hamasa ya kwenda hatua moja mbele katika kila mashindano,” amesema Rice, huku Arsenal ikisubiri mshindi wa jumla kati ya Manchester City au Newcastle United katika fainali ya Kombe la EFL, kombe walilolinyakua mara ya mwisho mwaka 1993.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *