Kongamano la wanataaluma lililohudhuriwa na maafisa kutoka Chama cha Kikomunisti cha China na chama kikubwa zaidi cha upinzani cha Kuomintang cha Taiwan lilifanyika China Februari 3. Vyombo vya habari vya Taiwan viliripoti kwamba lilikuwa kongamano la kwanza la aina hiyo kati ya vyama hivyo viwili katika kipindi cha miaka takriban tisa.
Kwa mujibu wa televisheni ya serikali ya China Central, watu takriban 100, wakiwemo wawakilishi kutoka sekta ya utalii, sayansi, teknolojia na nyanja zingine, walihudhuria kongamano hilo.
Song Tao, ambaye anaongoza Ofisi ya Masuala ya Taiwan ya Baraza la Serikali la China, alisisitiza kwamba pande hizo mbili lazima zipinge uhuru wa Taiwan na kukuza maendeleo ya amani ya uhusiano katika Mlango Bahari wa Taiwan.
Hsiao Hsu-tsen, makamu mwenyekiti wa Kuomintang, alisema akijibu kwamba uhuru wa Taiwan lazima upingwe na maendeleo ya amani yafuatiliwe pamoja.
Waangalizi wa mambo wanasema kwamba kwa kuendeleza mazungumzo na Kuomintang, China inaonekana kuwa na lengo la kudhibiti utawala wa Democratic Progressive Party, chama cha Rais wa Taiwan Lai Ching-te, kabla ya uchaguzi wa pamoja wa mitaa katika eneo la Taiwan mwaka huu na uchaguzi wa rais mwaka 2028. China inaona utawala wa Lai kama unaounga mkono uhuru.