Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Handeni Mkoani Tanga kimeweka mkazo mkubwa katika suala la elimu na uwajibikaji wa viongozi kama nguzo kuu za maendeleo ya jamii, wakati wa maadhimisho ya miaka 49 ya kuzaliwa kwa chama hicho yaliyofanyika katika Kata ya Mabanda.

Akizungumza kama mgeni rasmi, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Handeni, Amiri Ramadhani Changogo, amesena kuwa Serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imewekeza fedha za kutosha katika sekta ya elimu, hivyo ni wajibu wa wazazi, walezi na viongozi kuhakikisha watoto wote wanapata haki yao ya msingi ya elimu.

Changogo aliwataka wananchi kuwafichua watu wanaowazuia watoto kwenda shule au wanaohujumu juhudi za Serikali katika kuboresha elimu, akisisitiza kuwa CCM haitamvumilia mtu yeyote anayehusika na vitendo hivyo.

Aidha, amesisitiza uwajibikaji kwa viongozi wote katika kusimamia na kutekeleza miradi ya maendeleo, akibainisha kuwa chama hakitakuwa tayari kumfumbia macho kiongozi yeyote atakayesababisha uzembe au uzoloteshaji wa miradi ya maendeleo katika jimbo au kata.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *