
Ripoti ya kila mwaka iliyotolewa leo na Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch (HRW), inaonyesha kuwa mfumo wa kimataifa wa haki za binadamu uko hatarini.
Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo Philippe Bolopion amesema kwamba chini ya shinikizo lisilokoma kutoka kwa Rais wa Marekani Donald Trump na kudhoofishwa kila mara na China na Urusi, mfumo wa kimataifa unaoongozwa na kanuni umezidi kuporomoka na kutishia kubomoa muundo ambao watetezi wa haki za binadamu wamekuwa wakiutegemea kushinikiza viwango vya kulinda haki.
Amezihimiza serikali ambazo bado zinathamini haki za binadamu, pamoja na asasi za kiraia na taasisi za kimataifa, kuunda muungano wa kimkakati ili kukabiliana na mwenendo huo. Ripoti hiyo imesema utawala wa awamu ya pili wa Trump umegubikwa tangu mwanzo na ukiukwaji wa wazi wa haki za binadamu.