Ripoti ya shirika la Human Rights Watch imesema hali ya haki za binadamu duniani ni mbaya kuliko miaka mingi iliyopita. Human Rights Watch inasema mfumo wa kimataifa wa haki za binadamu uko katika hatari kubwa. Mkurugenzi mtendaji wa shirika hilo, Philippe Bolopion, amesema kuwa “mfumo wa haki za binadamu duniani uko kwenye ukingo wa kuporomoka.”
“Harakati za haki za binadamu ziko matatani. Ni kipindi hatari kwa haki za binadamu. Utawala wa Trump unashambulia mfumo wa dunia wa utaratibu wa kimataifa unaozingatia sheria kwa namna ambayo inaweza kwa kweli kudhoofisha harakati za haki za binadamu”, alisema Bolopion.
Ripoti hiyo yenye kurasa 529 imeikosoa vikali Marekani, ikielezea kuwa muhula wa pili wa Rais Donald Trump umeanza kwa vitendo vinavyoonyesha dharau kwa haki za binadamu. Shirika hilo linataja uvamizi wa maafisa wa uhamiaji wa Marekani, ICE, ambao unadaiwa kuwa wa vurugu na wa kikatili bila sababu, pamoja na kukamatwa kwa wanafunzi wa kigeni kutokana na kauli au misimamo yao ya kisiasa.
Shirika la Human Rights Watch linasema kuwa serikali ya Marekani inajaribu kudhoofisha taasisi za kimataifa zinazolenga kulinda haki za binadamu na kuwawajibisha wanaokiuka.
Nchini Urusi, Human Rights Watch inasema kuwa serikali ya Rais Vladimir Putin inaongeza mashinikizo dhidi ya wakosoaji wa Kremlin, ndani na nje ya nchi, huku vita dhidi ya Ukraine vikiendelea. Wapinzani wa kisiasa wanazidi kufungwa au kunyamazishwa kwa tuhuma zinazotajwa kuwa za uongo. Mwezi Novemba, Urusi iliitangaza HRW kama shirika “lisilotakiwa,” na hivyo kuzuia kazi zake nchini humo.
“Raia Wako Hatarini Mashariki mwa Kongo”
Kwenye Ukanda wa Maziwa Makuu, ripoti ya HRW imesema ukiukaji wa haki za binadamu dhidi ya raia umeongezeka sana mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ukihusisha jeshi la serikali na makundi yenye silaha. Ripoti hiyo inasema kuwa makundi kama M23 inayoungwa mkono na Rwanda yametekeleza uhalifu wa kivita, ikiwemo mauaji na ukatili wa kingono, huku jeshi la Kongo na washirika wake wa Wazalendo pia wakituhumiwa kwa uhalifu kama huo. Human Rights Watch imetaja hukumu ya kifo dhidi ya Joseph Kabila, rais wa zamani wa Kongo, kuwa ilichochewa kisiasa.
Human Rights Watch pia inasema kuwa Rwanda, Burundi, Kongo na Jamhuri ya Afrika ya Kati zimeendelea kukandamiza uhuru wa kisiasa na kiraia, ikiwemo vyombo vya habari, uhuru wa kujieleza na mikutano ya amani. Shirika hilo linazitaka taasisi za kikanda na kimataifa kushinikiza serikali kulinda raia na kuheshimu demokrasia.
Ubaguzi wa kijinsia uliokithiri
Huko Afghanistan, ripoti hiyo inazungumzia hali ya wanawake chini ya utawala wa Taliban, ikisema kuwa vizuizi vimeongezeka zaidi, ikiwemo marufuku ya vitabu vilivyoandikwa na wanawake katika vyuo vikuu na kukamatwa kwa wanawake kwa kukiuka sheria kali za mavazi. HRW sasa inaita hali hiyo “gender apartheid” yaani ubaguzi wa kijinsia uliokithiri.
Nchini Iran, HRW inaonya kuhusu idadi kubwa ya kunyongwa, kukamatwa kwa raia kwa wingi, na hukumu za kifo zinazotolewa hata kwa makosa ya dawa za kulevya au kesi za kisiasa zisizo za haki, hasa dhidi ya makundi madogo kama Wakurdi na Waarabu.
Ripoti hiyo pia inaonyesha kuwa chuki dhidi ya mashoga na watu wanaobadili jinsia inaongezeka katika nchi kadhaa, ikiwemo Marekani na Hungary. Hata hivyo, HRW inataja hatua chache chanya, kama vile nchi ya Saint Lucia katika eneo la Caribbean kuondoa sheria zinazoharamisha ushoga.
Aidha, shirika la Human Rights Watch linatoa wito kwa serikali zinazothamini haki za binadamu kushirikiana na mashirika ya kiraia na taasisi za kimataifa ili kuzuia kuporomoka kwa mfumo wa kimataifa wa haki na uhuru.