
WHO na IARC wamesema hayo katika ripoti yao mpya iliyotolewa kuenda sambamba na siku ya kuelimisha umma kuhusu ugonjwa wa saratani, maadhimisho ambayo hufanyika tarehe 4 ya mwezi Februari ya kila mwaka.
Ripoti yao iliyotolewa Februari 3, 2026 mjini Geneva nchini Uswisi na Lyon nchini Ufaransa, inajumuisha uchambuzi wa kwanza wa aina yake kuwahi kubaini kuwa asilimia 37 ya magonjwa yote mapya ya saratani ambayo ni sawa na wagonjwa milioni 7.1 yamehusishwa na sababu zinazoweza kudhibitiwa.
Sababu hizo ni pamoja na matumizi ya tumbaku, pombe, uzito uliopitiliza, na kwa mara ya kwanza maambukizi tisa yanayosababisha saratani yamejumuishwa.
Utafiti huo uliotumia takwimu kutoka nchi 185 umeitaja tumbaku kama chanzo kikuu kinachosababisha asilimia 15 ya magonjwa yote mapya, ikifuatiwa na maambukizi asilimia 10 na unywaji wa pombe asilimia 3. Saratani za mapafu, tumbo, na mlango wa uzazi zimechangia karibu nusu ya maambukizi yote yanayoweza kuzuilika duniani kote.
Dkt. André Ilbawi, ambaye ni kiongozi wa kikundi cha WHO cha kudhibiti saratani, amesisitiza umuhimu wa takwimu hizi akisema huu ni uchambuzi wa kwanza wa kimataifa unaoonesha kiasi gani cha hatari ya saratani hutokana na sababu zinazoweza kuzuilika.
Takwimu zinaonesha mzigo wa saratani zinazoweza kuzuilika ni mkubwa zaidi kwa wanaume ambapo ni asilimia 45 ikilinganishwa na wanawake asilimia 30, huku uvutaji wa sigara ukiwa sababu kuu kwa wanaume.
Katika ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara, mzigo huo kwa wanawake umefikia asilimia 38, kiwango ambacho ni kikubwa kuliko maeneo mengine kutokana na maambukizi kama virusi vya Saratani ya shingo ya Kizazi (HPV).
Dkt. Isabelle Soerjomataram kutoka IARC amebainisha kuwa kushughulikia sababu hizi zinazozuilika ni moja ya fursa zenye nguvu zaidi ya kupunguza mzigo wa saratani duniani.
Ili kukabiliana na hali hii, WHO imehimiza nchi kuimarisha hatua za udhibiti wa tumbaku, kanuni za pombe, na kutoa chanjo dhidi ya maambukizi yanayosababisha saratani kama vile HPV na Homa ya Ini aina B.
Halikadhalika kupunguza uchafuzi wa hew ana kuweka mazingira salama ya kazi.