Jeshi la Sudan limesema limeuvunja mzingiro wa miaka mingi katika mji wa Kadugli na hivyo kuleta ahueni kwa maelfu ya watu waliokuwa wanakabiliwa na njaa. Hatua hii ya sasa nchini Sudan inaashiria mabadiliko katika muelekeo wa vita vinavyoikumba nchi hiyo. 

Miji ya Kadugli na mji jirani wa al-Dalanj ilikuwa imezingirwa tangu kuanza kwa vita nchini Sudan kati ya majeshi ya serikali na vikosi vya RSF. Jeshi la Sudan limesema limeuvunja mzingiro huo katika mji wa Kadugli na wiki iliyopita iliudhibiti mji wa al-Dalanj.

Sudan | Wakimbizi wa Sudan kutokana na mashambulizi ya vikosi vya RSF
Watu wanaokimbia makazi yao kutokana na mashambulizi ya vikosi vya RSF nchini SudanPicha: REUTERS

Uwezekano wa kusonga mbele Jeshi la Sudan linaloongozwa na Abdel Fattah Al Burhan umetokana na kuvunjika kwa utaratibu wa mfumo wa usambazaji wa bidhaa za RSF kutokea nchini Libya hadi kwenye eneo la Kordofan, hayo ni kwa mujibu wa chanzo cha kijeshi na kutoka kwenye Kundi la SPLM-N la Harakati za Ukombozi wa Watu wa Sudan-Kaskazini lenye makao yake makuu katika majimbo ya Blue Nile na Kordofan Kusini.

Vyanzo hivyo hivyo viwili vimesema mafanikio ya jeshi la Sudan yametokana kwa kiasi kikubwa na mashambulizi ya ndege zisizo na rubani pamoja na mvutano wa ndani wa makundi yaliyojiunga na RSF.

Raia katika mji wa Kadugli washerehekea

Televisheni ya Sudan ilirusha picha za watu wa mji wa Kadugli waliokuwa wanasherehekea huku wanajeshi wakipita juu ya magari ya kijeshi.

Jenerali Abdel-Fattah al- Burhan amesema vikosi vya RSF vimefurushwa kutoka kwenye mji wa Kadugli, ambao ni mji mkubwa zaidi katika jimbo la Kordofan Kusini, na kwamba barabara kati ya mji huo na mji wa karibu wa Dilling imefunguliwa tena.

Sudan ilitumbukia katika machafuko mnamo mwezi Aprili mwaka 2023 baada ya kuzuka mzozo wa kugombea madaraka kati ya jeshi la serikali na vikosi vya RSF na kusababisha mapigano katika mji mkuu, wa Sudan, Khartoum ambayo yalienea hadi kwenye miji mingine nchini humo.

Vita hivyo vimesababisha vifo vya zaidi ya watu 40,000, kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa,ingawa mashirika ya misaada yanasema idadi hiyo ni Ndongo na kwamba inawezekana kuwa kubwa zaidi.

Vikosi vya kwa RSF vinanvyoongozwa na Muhammad Hamdan Dagalo, maarufu Hemedti vimekuwa vikipigana  na jeshi la Sudan kwa karibu miaka mitatu sasa.

Umoja wa Mataifau mesema mzingiro huo uliowekwa na wapiganaji wa RSF ulisababisha mji wa Kadugli kukaribia kutumbukia kwenye baa la njaa. Takriban watu 147,000 ambayo ni asilimia 80 ya idadi ya watu wa Kadugli walilazimika kukimbia mji huo.

Sudan | Wakimbizi wa Sudan kutokana na mashambulizi ya vikosi vya RSF
Watu wanaokimbia makazi yao kutokana na mashambulizi ya vikosi vya RSF nchini SudanPicha: REUTERS

Wakati huo huo Umoja wa Falme za Kiarabu umeahidi msaada wa dola milioni 500 kwa Sudan huku taifa hilo la Ghuba ikikabiliwa na mashtaka yanayohusu kuchochea mzozo huo.

Naye Mkuu wa Baraza la Wakimbizi la Norway (NRC) Jan Egeland, ameonya kwamba maelfu ya watu wako katika hatari ya kukabiliwa vifo katika eneo la Kordofan Kusini mwa Sudan, miezi michache tu baada ya kuanguka kwa jiji la El Fasher huko Darfur.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *