Akiwa anasafiri na ujumbe wa kibiashara kutoka Ujerumani,kituo cha kwanza cha Kansela huyo kitakuwa Saudi Arabia ambapo atakutana na Mwanamfalme Mohammed bin Salman, kisha aelekee Qatar na kumaliza ziara yake katika Umoja wa Falme za Kiarabu.
Katika ziara hiyo Kansela Merz analenga kuimarisha ushirikiano na mataifa hayo yenye kuzalisha gesi na mafuta, huku ushirikiano ukitarajiwa kuimarishwa zaidi katika sekta ya nishati.
Ulaya wapunguza utegemezi wa gesi ya Urusi
Kwa miongo kadhaa, mataifa hayo ya Ghuba yamekuwa yakiiuzia Ujerumani mafuta na tangu Urusi ianze uvamizi wake nchini Ukraine karibu miaka minne iliyopita, Qatar imekuwa na umuhimu mkubwa katika suala la kuisambazia Ujerumani gesi.
Umoja wa Ulaya umepunguza kwa kiasi kikubwa utegemezi wake kwa gesi ya Urusi, kwani kwa sasa Ujerumani inapata asilimia 10 tu ya gesi kutoka Urusi, huku Marekani ikiwa iliiuzia Ujerumani asilimia 30 ya gesi mwaka 2024.
Kulingana na serikali ya Ujerumani, kiasi hicho kinachosambazwa na Marekani na Urusi kwa Ujerumani, kinaweza kupungua zaidi iwapo kwa mfano, saudi Arabia na Qatar zitaiuzia Ujerumani gesi zaidi.
Mazungumzo ya Merz na viongozi wa mataifa hayo pia yatajikita katika mikataba ya silaha. Serikali zilizopita za Ujerumani zilichukua mwelekeo wa tahadhari lilipokuja suala la uuzaji wa silaha kwa nchi hizo za Kiarabu kutokana na masuala ya haki za binadamu na kuhusika kwa mataifa hayo katika mizozo ya kikanda. Lakini serikali ya Merz sasa, inataka kulegeza msimamo huu.
Kwa muda sasa, Ujerumani imekuwa ikiuza silaha na kusaini mikataba mikubwa ya miundo mbinu na mataifa ya eneo la Ghuba, ambayo badala yake yamekuwa yakitumia utajiri wake wa nishati kuekeza katika makampuni makubwa ya Ujerumani kama Volkswagen na Deutsche Bank.
Suala jengine muhimu litakalokuwa kwenye mjadala wa Kansela Merz na viongozi hao wa mataifa ya Ghuba ni hali jumla ya ndani na nje ya nchi zinazoizunguka Iran.
Maelfu waliuwawa maandamano ya Iran
Kumekuwa na hofu inayoongezeka kuhusiana na kuzuka kwa vita vipya katika siku za hivi karibuni, kwa kuwa Rais wa Marekani Donald Trump ameutishia mara kwa mara uongozi wa Iran kwamba ataushambulia kijeshi, baadhi ya sababu zikiwa vikosi vya usalama nchini humo kutumia nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji katika maandamano makubwa yaliyoshuhudiwa nchini humo hivi majuzi.
Inadaiwa kuwa maelfu au hata makumi kwa maelfu ya watu waliuwawa wakati wa maandamano hayo.
Jeshi la Marekani limeongeza pakubwa uwepo wake katika eneo hilo tangu mwanzoni mwa mwezi Januari, ila ripoti za hivi karibuni zinaeleza kuwa kutafanyika mazungumzo kati ya wawakilishi wa Marekani na Iran mnamo siku ya Ijumaa.
Chanzo: DPA/AFP/DW