
Waasi wa M23 wamekiri kuhusika na shambulizi la droni liliulolenga uwanja wa kimkakati wa ndege unaotumiwa na jeshi katika eneo la kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Katika taarifa yake ya leo, kundi la M23 linaloipinga serikali, limedai kuwa shambulizi hilo kati ya Jumamosi na Jumapili, liliharibu kituo cha kijeshi cha ndege za droni, kilichoko katika uwanja wa ndege wa Kisangani.
Utawala wa jimbo la Tshopo ambako Kisangani ndio mji mkuu, ulisema mapema Jumatatu kwamba droni zipatazo 8 za adui ziliharibiwa kabla ya kufikia malengo yake.
Madai hayo ya M23 yanatolewa kufuatia tangazo la Umoja wa Mataifa la kupeleka hivi karibuni ujumbe huko mashariki mwa Kongo, ili kusaidia kutekeleza makubaliano ya kusitisha vita ambayo yamekiukwa mara nyingi.