Mkuu wa Idara ya Taifa ya Uhamiaji na Ulinzi wa Mipaka nchini Marekani Tom Homan amesema Jumatano kwamba karibu maafisa 700 kati ya kama 3,000 wa shirikisho walioko Minnesota watarejeshwa.
Operesheni za kuwadhibiti wahamiaji ziliibua sintofahamu kwenye miji pacha ya St. Pauli na Minneapolis na kuchochea maandamano na hasa tangu baada ya mwandamanaji Alex Pretti kuuliwa, akiwa mtu wa pili kupigwa risasi na maafisa hao wa uhamiaji huko Minneapolis.
“Kwa kuzingatia kuimarika kwa ushirikiano, na kutokana na hitaji la maafisa wachache wa usalama wa umma kufanya kazi hii na mazingira salama, ninatangaza, kuanzia sasa, tutawarejesha watu 700 kuanzia leo — wafanyakazi 700 wa uhamiaji,” alisema Homan kwenye mkutano na waandishi wa habari.
Homan alisema wiki iliyopita kwamba idadi ya maafisa wa shirikisho itapunguzwa katika Jimbo la Minnesota, lakini hilo litatekelezwa tu ikiwa maafisa wa eneo hilo wataonyesha ushirikiano.
Magereza zatakiwa kutoa taarifa za wahamiaji waliokamatwa
Alitoa matamshi hayo baada ya Rais Donald Trump kuonyesha ishara ya utayari wa kulegeza hali ya mvutano Minneapolis na St. Pauli.
Homan aidha alizishinikiza magereza kutoa taarifa kwa maafisa hao wa uhamiaji – ICE – kuhusu wafungwa ambao wanaweza kufukuzwa nchini, akisema kuwahamishia kwao wafungwa kama hao ni salama zaidi kwa sababu inamaanisha kwamba maafisa wachache wanapaswa kuwepo kwenye maeneo mbalimbali wakiwatafuta watu wanaoishi nchini humo kinyume cha sheria.
Ikulu ya White House kwa muda mrefu imekuwa ikilalamikia matatizo wakati wa kuwakamata wahamiaji kwenye majimbo ambayo hayatoi ushirikiano na Wizara ya Mambo ya Ndani. Na alipoulizwa kuhusu hilo, Homan alisema anadhani operesheni za ICE kwenye jimbo la Minnesota zilikuwa za mafanikio.
“Ndio nimerekodi watu kadhaa ambao tumewakamata mitaani kwenye miji hiyo pacha, kwa hiyo nadhani imefanikiwa sana kwa kuzingatia usalama wa umma,” alisema Homan.
“Ilikuwa ni operesheni kamilifu? Hapana. Hapana. Tumeunda mlolongo wa kimamlaka ili kuhakikisha kwamba wote tunaelewana, na kuhakikisha kuwa tunafuata kanuni. Sidhani kama kuna mtu yeyote ambaye hakufanya kile alichopaswa kufanya kwa makusudi.”