Mama wa mwanamke Mjapani aliyetekwa nyara na Korea Kaskazini ameelezea matumaini ya kuungana tena na binti yake baada ya karibu miaka 50 ya kutengana.
Yokota Sakie anatimiza umri wa miaka 90 mnamo Februari 4. Yeye ndiye mzazi pekee aliyesalia wa mateka waliotambuliwa na serikali ya Japani ambao bado hawajulikani waliko.
Binti yake Megumi alitekwa nyara mwaka 1977 akiwa njiani kurudi nyumbani kutoka shuleni katika mji wa Niigata alipokuwa na umri wa miaka 13.
Akizungumza na NHK kabla ya siku yake ya kuzaliwa, Yokota alisema hawezi kuamini muda mrefu kama huo umepita.
Alisema anaanza kuwa dhaifu, lakini anatembea kila siku na kula chakula chenye lishe na anajaribu kujiweka sawa.
Alisema anajiuliza ni kwa nini hakuna maendeleo yaliyopatikana katika kutatua suala la utekaji nyara, ingawa amewaomba mara kwa mara mawaziri wakuu wa Japani kushughulikia suala hilo na wakamwambia kwamba watafanya hivyo.
Yokota alisema kwamba kuacha suala hilo bila kutatuliwa kunaifurahisha Korea Kaskazini, na pengine nchi hiyo inaidharau Japani. Aliongeza kuwa Japani inahitaji kuongeza diplomasia yake ili kuepuka kupoteza heshima.
Akisema kwamba watu wa Korea Kaskazini hawana uhuru au chakula cha kutosha kama wale wa Japani, Yokota alisema binti yake lazima anaishi kwa hofu lakini anashikilia matumaini.
Alisema anataka kumuona Megumi, ambaye sasa ni mwanamke mzee, japo mara moja tu.
Alisema hataki mtu yeyote aishi maisha kama yake, na anatumai waliotekwa nyara wote waliobaki watarudi nyumbani.