
Wakati ikisisitiza tena wito wake wa kusitishwa kwa uhasama, MONUSCO inakumbusha kuwa, kwa mujibu wa Azimio la Baraza la Usalama 2808 (2025), Ujumbe umepewa mamlaka ya wazi ya kuunga mkono utekelezaji wa usitishaji mapigano wa kudumu, ikiwemo kupitia ushiriki wake na utoaji wa msaada wa kiufundi na vifaa kwa Mkutano wa Kimataifa wa Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR) kupitia Mfumo wa Pamoja wa Uhakiki Uliopanuliwa Plus (EJVM+).
Katika taarifa iliyosambazwa tarehe 3 Februari kutoka jijini Kinshasa, MONUSCO inasema inakaribisha ushiriki endelevu wa Serikali ya Qatar, Marekani, Muunano wa Afrika na Mpatanishi wake, Jumuiya ya Afrika Mashariki, Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika, pamoja na Mkutano wa Kimataifa wa Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR). Unawahimiza kuendelea kudumisha na kuimarisha msaada wao kwa juhudi za amani na usalama mashariki mwa DRC.
Kwa kuzingatia mamlaka yake, MONUSCO imeimarisha utayari wake wa ndani kuunga mkono muundo wa ufuatiliaji na uhakiki wa usitishaji mapigano kwa njia ya hatua kwa hatua na inayoweza kubadilika kulingana na mazingira.
“MONUSCO iko tayari kuunga mkono mfumo wa kuaminika wa ufuatiliaji na uhakiki wa usitishaji mapigano, ndani ya mipaka ya mamlaka yake ya Baraza la Usalama na kwa heshima kamili ya uhuru wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Ujumbe utaendelea kushirikiana kwa njia chanya na wadau husika ndani ya muundo uliopo wa usitishaji mapigano na kuwasiliana kwa uwazi kuhusu upeo na namna ya msaada wake,” anasema Bi. Vivian van de Perre, Naibu Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa akihudumu pia kwa nafasi ya Naibu Mkuu wa MONUSCO.
MONUSCO inathibitisha tena dhamira yake ya kuunga mkono juhudi za kupunguza vurugu, kulinda raia, na kuweka mazingira ya suluhisho la kisiasa endelevu mashariki mwa DRC, kwa mujibu wa mamlaka yake.