
Shirikisho la Soka la Morocco, limesema kuwa litakata rufaa dhidi ya adhabu ya Dola 715,000 iliyopewa Senegal, kufuatia vurugu zilizojitokeza wakati wa mchezo wa fainali ya AFCON 2025, uliohusisha mataifa hayo mawili.
Katika taarifa yake iliyotolewa Februari 3, 2026, Morocco imesisitiza kuwa adhabu ya kamati ya nidhamu ya CAF waliyopewa Senegal haitoshi, kwani ‘haifanani’ na vitendo walivyovifanya wakati wa mchezo huo.
Kwa upande wake, Shirikisho la Soka la Senegal (FSF), limeweka wazi kuwa halina mpango wa kukata rufaa dhidi ya adhabu zao, ikisisitiza kuwa itawajibika kwa adhabu hizo kwa misingi ya kuheshimu kanuni na taratibu zilizowekwa na Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF).
Shirikisho la soka barani Afrika CAF limetoa adhabu kali kwa Senegal na Morocco kufuatia vurugu wakati wa fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika 2025.
Kocha Mkuu wa timu ya taifa ya Senegal Pape Bouna Thiaw alitozwa faini ya Dola 100,000, baada ya kuwaamuru wachezaji kutoka uwanjani.
Kwa upande wa wachezaji, Iliman Cheikh Baroy Ndiaye na Ismaila Sarr wamefungiwa kila mmoja mechi mbili rasmi za CAF kwa kuonesha utovu wa nidhamu kwa mwamuzi.