Katika miaka ya hivi karibuni, kumekuwa na msukumo mkubwa wa kitaifa na kimataifa wa kuhamasisha ushiriki wa wanawake katika siasa.

Hata hivyo, juhudi nyingi zimekuwa zikijikita zaidi katika vipindi maalumu vinavyokaribia uchaguzi mkuu, badala ya kuendeleza mchakato wa muda mrefu wa kuwajengea uwezo wanawake wanasiasa.

Hali hii imekuwa ikipunguza tija ya uwezeshaji huo na kuacha maswali kuhusu uendelevu na ubora wa ushiriki wa wanawake katika uongozi wa kisiasa.

Uhalisia unaonesha kuwa siasa si tukio la msimu, bali ni mchakato unaohitaji maandalizi ya muda mrefu, uzoefu, maarifa na mtandao mpana wa ushawishi.

Mwanamke anayetarajiwa kushiriki kwa ufanisi katika ulingo wa siasa anahitaji kujengewa uwezo wake katika vipindi vyote, si kusubiri kampeni za muda mfupi zinazolenga zaidi kushinda uchaguzi kuliko kujenga uongozi thabiti.

Mafunzo yanayotolewa wakati wa uchaguzi mara nyingi huwa ya haraka, ya juu juu na hayampi mwanamke nafasi ya kuimarisha misingi ya ujasiri, uelewa wa sera, mbinu za kisiasa na usimamizi wa shinikizo la kisiasa.

Kujengewa uwezo kwa wanawake wanasiasa kunapaswa kuwa endelevu na kugusa maeneo mbalimbali ikiwemo uongozi, mawasiliano ya kisiasa, usimamizi wa migogoro, uchambuzi wa sera, utafutaji wa rasilimali na matumizi ya teknolojia katika siasa za kisasa.

Mafunzo ya aina hii yakitolewa kwa muda mrefu huongeza uwezekano wa wanawake kujijenga kama viongozi wanaoaminika, wanaoheshimika na wanaoweza kushindana kwa haki katika majukwaa ya kisiasa bila kutegemea upendeleo au nafasi za viti maalumu pekee.

Aidha, uwezeshaji endelevu huondoa dhana potofu kwamba wanawake wanahitaji msukumo wa dharura kila inapokaribia uchaguzi. Badala yake, hujenga mtazamo kuwa wanawake ni wadau wa kudumu katika siasa wenye mchango muhimu katika kutunga sera, kusimamia utekelezaji wake na kuwakilisha maslahi ya jamii.

Hii pia husaidia kubadili fikra za jamii ambazo mara nyingi zimekuwa zikihusisha uongozi wa kisiasa na wanaume, huku wanawake wakionekana kama washiriki wa pembeni. Pia, kujenga uwezo nje ya vipindi vya uchaguzi kunawawezesha wanawake kujifunza kutokana na uzoefu wa vitendo.

Wanapata nafasi ya kushiriki katika mijadala ya kitaifa, kamati za kisiasa, mashirika ya kiraia na shughuli za kijamii zinazowaandaa kukabiliana na changamoto halisi za kisiasa.

Uzoefu huu hauwezi kupatikana kwa mafunzo ya siku chache yaliyojaa hamasa ya uchaguzi, bali kupitia ushiriki wa muda mrefu na unaoendelea. Zaidi ya hayo, Binafsi nalitazama hili kama ni uwezeshaji wa wanawake wanasiasa kwa mtazamo wa muda mrefu, ambao huchangia katika kuimarisha demokrasia jumuishi.

Uongozi unaoakisi makundi yote ya kijamii ikiwamo wanawake, huwa na uamuzi unaozingatia mahitaji halisi ya wananchi.

Tafiti mbalimbali zinaonesha kuwa wanawake viongozi huwa na msisitizo mkubwa katika masuala ya huduma za jamii, elimu, afya na ustawi wa familia, ambayo ni nguzo muhimu za maendeleo endelevu.

Kwa maana hiyo, ni muhimu kutambua kuwa uwezeshaji endelevu hujenga uthubutu wa wanawake katika kukabiliana na changamoto za kipekee wanazokutana nazo katika siasa, ikiwemo ukosefu wa rasilimali, unyanyapaa wa kijinsia, lugha ya matusi na mashambulizi ya kisaikolojia.

Wanawake wanaopata mafunzo ya muda mrefu hujifunza mbinu za kujilinda kisheria, kujenga taswira chanya mbele ya umma na kusimamia presha ya kisiasa bila kukata tamaa.

Kwa ujumla, ni muhimu kwa wadau wa siasa, serikali, vyama vya siasa na mashirika ya kiraia kubadili mtazamo wao kuhusu uwezeshaji wa wanawake wanasiasa. Badala ya kusubiri vipindi vya uchaguzi mkuu, juhudi zinapaswa kuelekezwa katika kujenga uwezo wao kwa wakati wote.

Hatua hii haitasaidia tu kuongeza idadi ya wanawake katika siasa, bali pia kuboresha ubora wa uongozi, kuimarisha imani ya wananchi katika demokrasia na kuweka msingi imara wa usawa wa kijinsia katika uongozi wa kisiasa.

Vilevile, uwezeshaji endelevu wa wanawake wanasiasa husaidia kujenga kizazi kipya cha viongozi wa kike wanaojifunza kupitia mifano halisi. Wanawake waliopata mafunzo na uzoefu wa muda mrefu wanakuwa walezi na washauri kwa wengine, hali inayochochea uendelevu wa uongozi wa wanawake ndani ya vyama vya siasa na taasisi za umma. Mfumo huu wa uongozi wa kurithishana uzoefu hupunguza utegemezi wa programu za dharura za uchaguzi na badala yake hujenga hazina ya maarifa na ujuzi inayodumu kwa muda mrefu.
Lakini jamii nayo inanufaika moja kwa moja pale wanawake wanasiasa wanapojengewa uwezo kwa misingi ya muda mrefu. Wanawake waliokomaa kisiasa huleta siasa zenye mwelekeo wa hoja, maadili na uwajibikaji, badala ya siasa za jazba na migawanyiko.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *