Miongoni mwa waathirika wa mgodi wa Rubaya, wapo wachimbaji wa Kongo, lakini pia watoto, wanawake wafanyabiashara, pamoja na raia wengine waliokuwapo eneo hilo wakati wa tukio.
Baadhi ya majeruhi walihamishwa kwenda vituo vya afya Rubaya, huku wengine wakilazimika kupelekwa Goma, safari ya masaa kadhaa kwa ajili ya matibabu maalum. Kwa mujibu wa mashuhuda mbalimbali, katika migodi hii ya uchimbaji usionzingatia kanuni za uchimbaji hakuna mkataba wa ajira, hakuna ulinzi wa kijamii, wala bima endapo ajali itatokea.
Wachimbaji wakatia tamaa huduma za uokozi
Mchimbaji huyu, ambaye hatutataja jina lake, amesema “Hata wahudumu wa shirika la Msalaba Mwekundu, ikitokea maporomoko, huchelewa na huja baadaye. Ni wachimbaji wenyewe tu ndio hujaribu kusaidiana kidogo. Na hiyo misaada inakuwa duni. Wapo walionusurika waliokuwa wamejeruhiwa vibaya ambao walitolewa chini ya matope baada ya siku mbili. Wengi hawajui kutoa huduma ya kwanza, hawana mafunzo yoyote. Wapo pale kwa ajili ya madini na pesa tu.”
Huko Rubaya, mgodi wa madini ya coltan umefungwa kwa muda, kwa maelekezo ya mamlaka za waasi walioko eneo hilo, ili kuruhusu uokoaji kuendelea na kutafuta miili chini ya kifusi.
Pale mhimili mkuu wa familia anapofariki au kubaki mlemavu wa kudumu, athari zake huonekana mara moja: hakuna tena kipato, hakuna matibabu, na wakati mwingine familia hukosa hata mahali pa kuishi.
Thimothée Mbuya, ni mwenyekiti wa shirika lisilo la kiserikali la Justicia Asbl, linalotetea haki za binadamu na haki za mazingira katika mikoa yenye madini ya Haut-Katanga na Lualaba.
Wachimbaji wananufaikaje na madini ya coltan?
“Mchimbaji wa Kongo anaonekana leo kama mtu aliye peke yake, anayejitolea maisha yake. Kwa upande wa sheria na haki, hakuna hata uchunguzi unaoanza ili kujua ni nani warithi au familia za waathirika. Hakuna uchunguzi kabisa, na kila kitu huishia kwenye mazishi. Mara tu watu wanapozikwa, kesi inafungwa, inafungwa kabisa.”
Huko Rubaya, uchimbaji wa madini adimu ya Coltan unafanyika katika mazingira hatari sana: mashimo hayajawekwa nguzo za kuyaimarisha, hakuna mifumo ya kutoa maji, vifaa vya wachimbaji ni vichache au havipo, na hakuna udhibiti wa kiufundi. Zaidi ya hayo, eneo hilo liko chini ya usimamizi wa kundi la waasi la M23
Alex Kopp, afisa wa utetezi katika shirika la kimataifa la Global Witness, anaamini kuwa wajibu wa mkasa wa Rubaya unazihusisha pande zote.
“Waasi wa M23 wanaudhibiti moja kwa moja mji wa Rubaya na wanapaswa kuchukua hatua za usalama. Halafu kuna makampuni makubwa yanayonunua madini yanayotoka kwenye eneo hilo. Na mwisho, kuna nchi ambazo zina wajibu kuhusu hali ya sasa iliyoko katika eneo hilo.”
Taasisi ya serikali ya Huduma ya Usaidizi na Ufuatiliaji wa Uchimbaji Mdogo na wa Kongo (SAEMAPE) inatangaza kuwa serikali ya Kongo inatarajiwa hivi karibuni kutoa bima kwa vyama vya wachimbaji madini wa Kongo.
Mkurugenzi wake mkuu, Jean-Paul Kapongo, ameiambia DW kuwa mchakato huo tayari umeanza katika mikoa miwili ya majaribio: Haut-Katanga na Lualaba. Lakini katika uhalisia wa eneo la Rubaya, kama ilivyo sehemu nyingine za nchi, maelfu ya familia bado zinaendelea kufanya kazi bila ulinzi wowote wala mfumo wa msaada wa kijamii.
