Maelezo yaliyotolewa na maafisa wa Palestina na wa Umoja wa Mataifa yanaonyesha kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel unakataa kutekeleza awamu ya pili ya makubaliano ya kusitisha mapigano huko Ghaza.
Ghazi Hamad, afisa mwandamizi wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS amesisitiza kuwa, utawala wa Kizayuni hautaki kutekeleza awamu ya pili ya makubaliano ya kusitisha vita. Hamad amesema: “utawala ghasibu hautaki wasafiri wanaoingia na kutoka Ghaza wafanye hivyo kwa urahisi.”
Haitham Abdu, mjumbe wa ofisi ya kisiasa ya Harakati ya Wananachi kwa ajili ya Ukombozi wa Palestina, (Popular Front for the Liberation of Palestine) PFLP, yeye amezungumzia kushadidi kwa mashambulizi ya utawala wa Kizayuni dhidi ya Ghaza na akasema: “mashambulizi haya yanaonyesha jinsi wazayuni maghasibu wanavyoyadharau makubaliano ya kusitisha mapigano, wasivyokuwa na utashi wa kuingia katika awamu ya pili ya makubaliano hayo na namna wanavyochukua hatua za kuyahujumu na kuyakwamisha.”
Francesca Albanese, Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya haki za binadamu katika maeneo ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu na Israel, yeye pia amesisitiza kwamba utawala wa Kizayuni unapaswa ukomeshe kuikalia kwa mabavu ardhi ya Palestina. Albanese ameweka ujumbe kwenye mtandao wa kijamii wa X, ambapo mbali na kutilia mkazo ulazima wa kuheshimiwa maamuzi ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki ICJ, ametoa wito pia wa kuwepo ulinzi na uungaji mkono wa kibinadamu kwa wakazi wa Ghaza na hakikisho la kuingizwa misaada katika eneo hilo bila ya masharti yoyote.
Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Masuala ya Kibinadamu Tom Fletcher, yeye amezungumzia kufunguliwa tena kivuko cha Rafah na kusisitiza kwamba, kufunguliwa sehemu ya kivuko hicho ni hatua nzuri, lakini haitoshi. Fletcher amesema: “kivuko cha Rafah lazima kiwe kivuko cha huduma za kibinadamu kwa maana halisi ili tuweze kuharakisha upelekaji misaada”.
Awamu ya kwanza ya makubaliano ya kusitisha vita huko Ghaza iliidhinishwa utekelezaji wake mjini Sharm el-Sheikh, Misri Oktoba 10, 2025; makubaliano ambayo yalikuwa matokeo ya mazungumzo yasiyo ya ana kwa ana kati ya Hamas na utawala wa Kizayuni kwa upatanishi wa Misri, Qatar, Marekani, na Uturuki.
Katika muendelezo wa mchakato huo, mnamo Oktoba 13, 2025, Hamas iliwaachilia mateka wote 20 wa Kizayuni walio hai, na baadaye ikakabidhi miili ya mateka wengine kadhaa. Mkabala wake, utawala wa Kizayuni uliwaachilia huru mateka wapatao elfu mbili wa Kipalestina uliokuwa ukiwashikilia kwenye magereza yake.
Msimamo wa utawala wa Kizayuni wa kuendeleza hali mbaya ya kibinadamu na vita dhidi ya Gaza, na kukiuka wajibu wake wa kutekeleza awamu ya pili ya usitishaji mapigano ni matokeo ya kuongezeka migogoro ya ndani ya utawala huo na kushindwa baraza la mawaziri la waziri mkuu Benjamin Netanyahu kukabiliana na wazayuni wenye misimamo mikali ya kufurutu mpaka.
Baraza la mawaziri la Netanyahu limeundwa na mirengo miwili ya washupalia vita na wazayuni wenye misimamo ya kufurutu mpaka, ambao hawako tayari kukomesha operesheni za mashambulizi ya kijeshi huko Ghaza, wakiamini kwamba kuendeleza vita ni jambo la lazima.
Baada ya miezi kadhaa ya vita, baraza la mawaziri la Netanyahu limekabiliwa na hali ya kutoaminika mbele ya umma na mpasuko mkubwa wa kijamii. Hali mbaya ya mgogoro katika ardhi za Palestina zilizopachikwa jina bandia la Israel imesababisha madhara makubwa kwa wazayuni; lakini upinzani dhidi ya matakwa ya wazayuni wenye misimamo mikali, nao pia umeliweka katika hali mbaya baraza la mawaziri la Netanyahu.
Baraza la mawaziri la Netanyahu ni moja ya miuungano tete na dhaifu zaidi kuwahi kushuhudiwa katika miaka ya karibuni ndani ya utawala wa kizayuni. Netanyahu anategemea sana uungaji mkono wa vyama vya siasa vya kizayuni vyenye misimamo ya kufurutu mpaka; mirengo ambayo inaitakidi kuwa kusitisha mapigano ni ushindi kwa Muqawama wa Palestina. Kwa hiyo, kulegeza msimamo kwa namna yoyote ile kwa kuamua kutekeleza ahadi, iwe ni kwa kuwaachilia huru wafungwa Wapalestina, kukomesha mashambulizi au kuondoka kwenye kivuko cha Rafah kunaweza kuharakisha kuanguka kwa serikali ya Netanyahu.

Utawala wa Kizayuni unajaribu kuendeleza vita huko Ghaza ili kuchelewesha kushindwa kwake, katika hali ambayo gharama za vita hivyo zimeongezeka kwa kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa, huku kupotea itibari na uhalali wa kisiasa katika uga wa kimataifa kukiiweka Tel Aviv kwenye hali ngumu zaidi. Kuendelea kwa hali hiyo na kupamba moto tofauti za ndani ya utawala wa kizayuni, kutaandaa mazingira ya msambaratiko wa kisiasa na uchaguzi wa mapema, na hilo litamfanya Netanyahu alazimike kujiuzulu.
Kwa upande wa uga wa kimataifa pia, kuendelea utawala wa kizayuni kupuuza sheria za kimataifa na maazimio ya Umoja wa Mataifa kutakabiliwa na mijibizo ya jamii ya kimataifa na watetezi wa Palestina duniani kote. Kutengwa kisiasa Tel Aviv kunaweza kufungua njia ya uwekaji vikwazo zaidi vya kiuchumi vyenye malengo maalumu dhidi ya utawala wa Kizayuni.
Kutolewa pia hati na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC za kukamatwa Netanyahu na waziri wake wa zamani wa vita Yoav Gallant, kutafungua njia ya kufuatiliwa katika mahakama za kimataifa kesi za mauaji na mauaji ya kimbari yaliyofanywa na viongozi wa utawala huo…/