Kwa sasa, nchi muhimu zaUkanda wa Ghuba—Saudi Arabia, Qatar na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE)—zina nafasi ya juu katika vipaumbele vya serikali ya Ujerumani. Hili linaonekana wazi hata kwenye viwanja vya ndege vya miji mikuu yao. Hivi karibuni, Waziri wa Mazingira wa Ujerumani, Carsten Schneider, alitembelea Saudi Arabia, kisha ndege iliyombeba Waziri wa Uchumi, Katherina Reiche, ikatua nchini humo.

Waziri huyo alieleza sababu ya ziara hizo akisema: “Wakati ushirikiano ambao tumekuwa tukitegemea kwa miongo kadhaa unaanza kudhoofika, tunalazimika kutafuta washirika wapya.” Washirika hao wanahitajika hasa katika sekta za nishati na miradi ya kijeshi.

Ndiyo hasa anachofanya wiki hii Kansela wa Ujerumani, Friedrich Merz. Kuanzia Februari 4 hadi 6, anafanya ziara ya haraka katika nchi tatu za Ghuba: kwanza Saudi Arabia, kisha Qatar, na mwisho Umoja wa Falme za Kiarabu. Ziara zote hizi zinafanyika ndani ya muda usiozidi saa 72.

Lengo ni kuimarisha mahusiano ya kiuchumi na kusaini mikataba ya kuaminika, katika kipindi ambacho haijulikani tena kwa uhakika ni kwa kiasi gani Ulaya, na Ujerumani yenyewe, zinaweza kuendelea kuitegemea Marekani kama mshirika wao mkuu.

Kwanza India, sasa Ukanda wa Ghuba, na baadaye China

Ndiyo mwelekeo wa sasa wa diplomasia ya Ujerumani. Ndani ya Ofisi ya Kansela, kunazungumziwa kwa msisitizo suala la “ushirikiano mpya wa kimkakati” —ikiwa ni pamoja na India, ambako Kansela tayari ametembelea mapema mwaka huu, na China, ambayo Friedrich Merz anapanga kuitembelea mwishoni mwa Februari. Katikati ya ziara hizo mbili, sasa kuna safari ya Ukanda wa Ghuba.

Neno muhimu katika uhusiano wa Ujerumani na nchi za Ghuba ni nishati. Kwa miongo mingi, nchi za Ghuba zimekuwa wasambazaji wakuu wa mafuta kwa Ujerumani, ambayo haina rasilimali nyingi za asili. Tangu Urusi ilipoanzisha vita dhidi ya Ukraine, suala la gesi limekuwa muhimu zaidi.

Sehemu ya gesi kutoka Urusi katika Umoja wa Ulaya imepunguzwa kwa kiasi kikubwa. Hivi sasa, gesi ya kimiminika (LNG) inachangia takribani asilimia 10 ya matumizi ya gesi nchini Ujerumani, na mwaka 2024, karibu asilimia 30 ya LNG hiyo ilitoka Marekani. Serikali ya Ujerumani inaona ni vyema kupunguza utegemezi huo, kwa kupata gesi zaidi kutoka nchi kama Saudi Arabia na Qatar.

Kituo cha nishati cha “Deutsche Ostsee” katika bandari ya Mukran
Kituo cha nishati katika bandari ya Mukran: Gesi ya majimaji inaendelea kuwa muhimu zaidi kwa mahitaji ya nishati ya UjerumaniPicha: Stefan Sauer/dpa/picture alliance

Gesi kwa Ujerumani, silaha kwa nchi za Ghuba

Mwandishi mkuu wa DW, Michaela Küfner, anasafiri pamoja na Kansela Merz katika ziara yake ya Ukanda wa Ghuba. Akizungumza kuhusu suala la gesi, Kansema Merz anasema: “Kwa sasa, Washington ndiyo msambazaji mkubwa zaidi wa gesi ya kimiminika (LNG) barani Ulaya. Kama Ulaya haitaki kuacha utegemezi wa Urusi na kuingia moja kwa moja kwenye utegemezi wa Marekani, basi inahitaji wauzaji wa jadi wa nishati kutoka Mashariki ya Kati. Hii ina maana pia kwamba Ulaya, na Ujerumani hasa, huenda zikalazimika kulegeza masharti yake kuhusu mauzo ya silaha.”

Miradi mahsusi ambayo serikali itajadili katika ziara hiyo haikutajwa wazi kabla ya safari kuanza.

Hata hivyo, inajulikana kuwa nchi kama Saudi Arabia na Qatar zinaonesha nia ya kununua ndege ya kijeshi ya Airbus chapa A400M. Aidha, miradi mingi ya nishati haikufanikiwa hapo awali kwa sababu ya tofauti za msimamo: Qatar ilitaka mikataba ya muda mrefu ya usambazaji wa gesi, huku Ujerumani ikipendelea mikataba ya muda mfupi. Sasa, vyanzo vya serikali ya Ujerumani vinasema iko tayari kuwa rahisi zaidi na kukubaliana na masharti ya nchi za Ghuba.

Kansela Merz ataandamana na ujumbe mkubwa wa wafanyabiashara, lakini mjini Berlin waandishi wa habari pia wanataka kujua iwapo atazungumzia hali nyeti ya haki za binadamu katika nchi hizo tatu. Akijibu suala hilo wiki iliyopita, msemaji wa serikali, Stefan Kornelius, alisema: “Tumeona kwamba Saudi Arabia imeanza mwelekeo wa mageuzi, ikiwemo kufunguka zaidi kijamii na kitamaduni. Hii imeleta pia maboresho fulani katika haki za wanawake. Hata hivyo, bado kuna mengi ya kufanyika, na maboresho zaidi yanahitajika.”

India, Ahmedabad 2026 | Waziri Mkuu Modi na Kansela wa Ujerumani Merz katika Tamasha la Kimataifa la kurusha vishada
Washirika wapya—na wa zamani—wanaotaka biashara inayozingatia sheria, Kansela tayari aliwatafuta nchini India; hapa akiwa na Waziri Mkuu Modi tarehe 12 Januari wakati wa sherehe ya kurusha vishadaPicha: Shammi Mehra/AFP/Getty Images

Mvutano kuhusu “Baraza la Amani” la Trump

Mvutano unaohusiana na maandamano makubwa ya wananchi nchini Iran nao unaendelea kuathiri hali ya kisiasa katika eneo hilo. Kuna maswali kama Marekani itaamua kuingilia moja kwa moja na kuunga mkono upinzani ili kuuangusha utawala wa viongozi wa kidini. Aidha, vita vinavyoendelea katika Ukanda wa Gaza na sera za Marekani kuhusu mgogoro huo vinaendelea kuwa mada nyeti.

Hivi karibuni, Israel ilionyesha hasira yake baada ya kutangazwa kuwa Qatar itakuwa miongoni mwa wanachama wa “Baraza jipya la Amani” la Rais wa Marekani, linalolenga kutafuta suluhu ya mgogoro wa Gaza. Hatua hiyo ilizua mjadala na vichwa vya habari vingi.

Ujerumani haioni baraza hilo kama suluhu bora, hasa kwa sababu limeundwa waziwazi kama mbadala wa Umoja wa Mataifa ulioko New York. Akizungumzia suala hilo, msemaji wa serikali ya Ujerumani, Stefan Kornelius, alijibu kwa tahadhari akisema: “Muundo wa baraza hili unaongozwa na vigezo ambavyo hatuwezi kuvidhibiti wala kuvitathmini kwa kina. Tunaufahamu msimamo wa Israel, lakini pia tunajua kuwa Israel ina nia ya kuwa na uhusiano wa maelewano na Qatar. Haya ni mahusiano yanayoendelea kujengwa kati ya nchi husika, na Ujerumani haina nafasi ya kutoa maoni kwa sasa.”

Mfano huu unaonyesha jinsi eneo hili bado lilivyo nyeti kwa Ujerumani, na kwa nini kila neno la Kansela litafuatiliwa kwa makini mkubwa, licha ya msisitizo mkubwa kuwekwa kwenye ushirikiano wa kiuchumi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *