Rais wa Iran Masoud Pezeshkian anasema amemwagiza Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo kuendelea na mazungumzo na Marekani.
Alisema katika taarifa ya mitandao ya kijamii Februari 3 kwamba “Kwa kuzingatia maombi kutoka kwa serikali rafiki katika eneo hilo kujibu pendekezo la mazungumzo la Rais wa Marekani,” alimwagiza waziri wa mambo ya nje “kufuatilia mazungumzo ya haki na usawa.”
Hapo awali, vyombo vya habari vya Marekani viliripoti kwamba mjumbe maalum wa Rais Donald Trump wa Marekani Steve Witkoff na mkwewe Trump Jared Kushner wanatarajiwa kukutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi mjini Istanbul nchini Uturuki, Februari 6.
Vyombo hivyo vya habari pia viliripoti kwamba Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Qatar, Misri na baadhi ya nchi zingine huenda wakahudhuria.
Utawala wa Trump umetuma meli ya kubeba ndege ya USS Abraham Lincoln inayoendeshwa kwa nguvu za nyuklia kwenda Mashariki ya Kati ili kuongeza shinikizo kwa Iran kukubali kufanya mazungumzo kuhusu mpango wake wa nyuklia.
Ikiwa maafisa waandamizi kutoka Marekani na Iran watakutana, itakuwa ni mara ya kwanza tangu jeshi la Marekani kushambulia vituo vya nyuklia vya Iran mnamo Juni 2025.