Dar es Salaam. Mitandaoni kumekuwa na maswali mengi kwa nini Alikiba amesaini msanii wa kike kutoka Rwanda, Mutima Wangu ilihali Tanzania kuna wasanii wengi wa kike wanaofanya vizuri.
Kila mmoja anaongea lake wengine wanasema Alikiba ameukubali uwezo wa mwanadada huyo anayetamba na ngoma ya ‘King’ang’anizi’, wengine wanaamini alimsaini kibiashara.
Hatua hiyo imeendelea kuzua mijadala na maswali mengi katika tasnia ya burudani. Wengi wamejiuliza kwa nini msanii kutoka nje ya Tanzania? Kwa nini msanii wa kike? Na kwa nini sasa?
Ikumbukwe huyu ni msanii wa kwanza wa kike kutambulishwa Kings Music na awali waliowahi kusainiwa wote walikuwa wa kiume, Tommy Flavour, Country Wzizzy, Killy Music, K2ga, Cheed ambao hawakudumu muda mrefu wakaondoka na sasa Vanillah.
Mwananchi linakuletea baadhi ya sababu za Kiba kumsaini Mutima Wangu.
Kwanza kilichoivutia lebo ya Kings Music kumsaini Mutima Wangu ni kipaji chake. Mwanadada huyo ana sauti yenye hisia nzito na uwezo wa kuwasilisha maudhui ya mapenzi kwa uhalisia.
Sauti yake laini yenye ladha ya soul na Afro-pop, inaendana kwa karibu na falsafa ya muziki wa Alikiba ambaye kwa muda mrefu amejijengea jina kama kinara wa nyimbo za mapenzi Afrika.
Kwa Alikiba kusaini msanii si suala la idadi ya wafuasi mitandaoni pekee bali ni kipaji kinachodumu kwa muda mrefu. Mutima Wangu ana vigezo hivyo kuanzia sauti, uwezo wa kuandika na kuimba kwa hisia.
MKAKATI WA AFRIKA MASHARIKI
Katika miaka ya hivi karibuni, Alikiba ameonyesha anafanya muziki na kuangalia zaidi soko nje ya Tanzania. Kumsaini Mutima Wangu kutoka Rwanda ni hatua ya kimkakati ya kuimarisha uwepo wake katika soko la Afrika Mashariki na Kati.
Rwanda ni moja ya nchi zenye ukuaji mkubwa wa tasnia ya burudani, huku muziki wake ukianza kusambaa nje kwa kasi. Kupitia Mutima Wangu, Kiba anajenga daraja la muziki kati ya Tanzania na Rwanda jambo linalofungua milango ya kufanya shoo, ushirikiano na kuvuta mashabiki wapya.
UWEKEZAJI KWA WASANII WA KIKE
Licha ya vipaji vingi wasanii wa kike Afrika Mashariki bado wanakumbana na changamoto ya kukosa uwekezaji wa muda mrefu, usimamizi mzuri na mipango ya kimkakati.
Kiba kama msanii aliyepitia changamoto hizo kwa njia yake mwenyewe anaelewa kwa undani mapungufu ya mfumo uliopo, hivyo inakuwa rahisi kuwekeza kwake kwa sababu tayari ana uzoefu.
Kumsaini Mutima Wangu ni wazi wasanii wa kike nao wanastahili kuwekewa mkakati wa kitaalamu, si wa muda mfupi. Ni uwekezaji wa vipaji.
UZOEFU WA KIBA
Kiba amedumu kwenye tasnia kwa zaidi ya muongo mmoja, akishuhudia mabadiliko ya ladha ya muziki, mapinduzi ya kidijitali na changamoto za mikataba. Uzoefu huo unampa uwezo wa kumlea msanii kutoka hatua ya awali hadi ngazi ya kimataifa.
Kwa Mutima Wangu kusainiwa na Kiba ni sawa na kuingia darasani kwa mwalimu aliyefundisha vitendo na si nadharia. Kwa Kiba ni fursa ya kutumia uzoefu wake kuunda nyota mpya.
Mutima Wangu ana uwezo wa kuimba kwa Kinyarwanda, Kiswahili, Kiingereza na Kifaransa jambo linalompa nafasi kubwa ya kuvuka mipaka bila vikwazo vya lugha. Hii inaendana na maono ya Kiba ya kutengeneza muziki unaoeleweka katika maeneo tofauti ya Afrika na nje ya bara.
Kwa muziki wa dunia, lugha si kikwazo kikubwa tena, bali ladha na hisia za muziki nyota huyo ana vigezo hivyo.
Kwa jumla, kumsaini Mutima Wangu ni uamuzi unaounganisha kipaji, biashara ya muziki, upanuzi wa soko na dhamira ya kubadili taswira ya uwekezaji kwa wasanii wa kike Afrika Mashariki.
Endapo mradi huu utasimamiwa kwa weledi na uvumilivu, unaweza kuwa mfano bora wa ushirikiano wa kuvuka mipaka na kubeba mafanikio ya muda mrefu kwa pande zote mbili.
MSIKIE MWENYEWE
Meneja mpya wa Kings Music, Benjamin Olwal ambaye ni raia wa Kenya anasema lebo hiyo imejipanga kuwekeza zaidi kimataifa, lakini kwa sasa wataanza na Afrika Mashariki.
“Nimefanya kazi kwa karibu na Ali Kiba, naelewa malengo yake na kwa sasa lengo letu ni kuhakikisha tunawekeza nje zaidi na kupata madili huko kwa sababu muziki sasa umebadilika.”