Taasisi za fedha nchini zimehimizwa kufanya uwekezaji kwa wajasiriamali na wabunifu wa bicha za kidijitali ambao wamejikita katika biashara ya nishati safi ya kupikia ili kuchangia katika ufikiwaji wa ajenda ya serikali ya kuhakikisha ifikapo mwaka 2034 angalau asilimia 80 ya wananchi kutumia nishati safi.
Wito huo umetolewa Naibu Waziri wa Nishati, Salome Makamba katika uzinduzi wa mradi wa nishati safi ya kupikia katika shule ya sekondari Bunge Wasichana iliyopo mkoani Dodoma.
“Tanzania imepiga hatua kubwa katika ajenda ya Nishati Safi ya Kupikia, matumizi ya nishati hii yameongezeka kutoka asilimia 6.9 mwaka 2021 na kufikia asilimia 23.2 mwaka 2025. Hata hivyo, bado takribani asilimia 77 ya kaya nchini zinatumia nishati isiyo safi ya kupikia, hivyo taasisi za fedha zina fursa mbalimbali za kusaidia mafanikio haya kwa kushirikiana na Serikali katika maeneo ya pembezoni na yale ya vijijini.” Amesema Naibu Waziri Salome
Sambamba na hilo Naibu Waziri amewasisitiza wasambazaji wa gesi za mitungi kuongeza vituo vya usambazaji na ujazaji wa gesi za mitungi ili kurahisisha upatikanaji wake kwa watumiaji wengi zaidi, pia Wabunifu na vijana walioko vyuoni kufanya tafiti na kubuni nyenzo na teknolojia zitakazowezesha ajenda hii kusambaa na kuwafikia watu wengi.
Mradi wa gesi uliozinduliwa katika shule ya sekondari Bunge Wasichana ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la serikali kwa taasisi zinazohudumia chakula kwa watu zaidi ya 100 kutumia nishati safi ya kupikia ili kulinda afya za binadamu na kutunza mazingira.
Shule ya Sekondari ya Bunge Wasichana ina wanafunzi 555 na amekuwa ikitumia wastani wa Shilingi milioni 10.5 kwa kila miezi mitatu kununua kuni.
Mhariri @moseskwindi