Haya ni kulingana na mwakilishi wa biashara wa Marekani Jamieson Greer.
Katika taarifa yake, Greer amesema ofisi yake itashirikiana na bunge la Marekani mwaka huu kuhakikisha kwamba mpango huo unatoa fursa zaidi za masoko kwa biashara za Marekani, wakulima na wafugaji kwa ajili ya kuendana na sera ya Marekani Kwanza ya Rais Donald Trump.
Mpango unaohusisha nchi 32 za Afrika
Ukiwa ndio msingi wa biashara kati ya Marekani na Afrikakwa kipindi cha miaka 25, mkataba wa AGOA umeipa Marekani fursa ya kununua bidhaa za mabilioni ya dola bila ushuru kutoka nchi kadhaa za Afrika kila mwaka. Miongoni mwa bidhaa hizo ni magari na nguo.
Ila mpango huo ambao unahusisha nchi 32 za Afrika, ulifika mwisho Septemba mwaka jana na kuathiri maelfu ya kazi na kusababisha wafanyabiashara wanaouza bidhaa zao Marekani kukabiliwa na ushuru mkubwa kwa bidhaa zao.
Kulingana na Tume ya Biashara ya Marekani, USITC, mwaka 2024, Afrika iliiuzia Marekani bidhaa zenye gharama ya zaidi ya dola bilioni 8 chini ya mkataba huo ambapo nusu ya bidhaa hizo zilitokea Afrika Kusini hasa magari, madini na bidhaa za kilimo. Nigeria pia ilichangia kwa kuuza hasa mafuta na bidhaa zinazotokana na mafuta.
Mkataba huo wa AGOA unaotoa fursa ya kusaidia ukuaji barani Afrika ulipokwisha Septemba mwaka uliopita, hata mataifa madogo madogo ya Afrika yaliathirika. Kwa mfano sekta ya nguo ya Lesotho ambayo ndiyo inayotoa kiasi kikubwa cha ajira nchini humo, ilipata pigo baada ya mamia ya wafanyakazi kuachishwa kazi na kusababisha maandamano mwishoni mwa mwezi Oktoba.
Nchi lazima zioneshe kutii utawala wa sheria
Lesotho ambayo Trump aliielezea kuwa ni “sehemu ambayo hakuna mtu ambaye ameshawahi kuisikia” iliiuzia Marekani bidhaa zenye thamani ya dola milioni 150 chini ya mkataba wa AGOA mwaka 2024.
Kulingana na mwakilishi wa biashara wa Marekani, Greer, ili kufuzu kuingia katika mpango huo wa AGOA, mataifa ya Afrika ni sharti yaoneshe mwendelezo wa kupiga hatua za kuwa na uchumi unaotegemea soko, ni sharti ziwe zinafuata utawala wa sheria na ziondoe vigingi katika biashara na uwekezaji wa Marekani.
Vile vile nchi hizo zinastahili kubuni sera za kuhakikisha kuwa zinapunguza umaskini, kupambana na ufisadi na kuzilinda haki za binadamu.
Vyanzo: AFP/Reuters