Zanzibar. Magonjwa yasiyoambukiza yanazidi kuwa tishio kwa afya ya jamii nchini Tanzania, huku shinikizo la damu na kisukari vikiwa miongoni mwa magonjwa yanayowakumba zaidi wananchi, mara nyingi yakigundulika wakiwa tayari wagonjwa wapo katika hatua za hatari.

Changamoto hiyo pia inawakumba wakazi wa Zanzibar, imepelekea Vodacom Tanzania Foundation kuanzisha makambi ya afya bure kwa mara ya kwanza visiwani humo.

Kambi hiyo iliyoanza jana Februari 3 hadi 6, 2026, inalenga kutoa huduma za uchunguzi wa mapema, ushauri wa kitaalamu na elimu ya kinga dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza (NCDs), hatua ambayo inatarajiwa kupunguza madhara makubwa ya kiafya kwa jamii.

Mkutano wa ufunguzi rasmi wa kambi hiyo umeanyika leo Jumatano, Februari 4, 2026 na kuhudhuriwa na Mkurugenzi wa Huduma za Tiba wa Wizara ya Afya Zanzibar, Dk Msafiri Marijani, umeonesha wazi umuhimu wa juhudi za kinga na uchunguzi wa mapema.

“Shinikizo la damu na kisukari vinaathiri wananchi wengi Zanzibar, mara nyingi bila dalili za awali. Mpango kama huu unaowawezesha wananchi kuchukua hatua mapema ni muhimu sana katika kudhibiti magonjwa haya na kuzuia madhara makubwa kiafya,” amesema Dk Marijani.

Takwimu zinaonyesha ongezeko la kasi la magonjwa yasiyoambukiza nchini Tanzania, huku ugonjwa wa shinikizo la juu la damu ukiongoza kwa asilimia 47.

Shinikizo la damu na kisukari ni mojawapo ya magonjwa yasiyoambukiza yanayoonekana mara kwa mara kwenye vituo vya afya nchini Tanzania katika mwaka 2024.

Meneja wa Vodacom Tanzania Foundation, Sandra Oswald, amesema kambi hizi zina lengo la kusogeza huduma za afya karibu na wananchi na kuongeza upatikanaji wa uchunguzi wa kinga katika jamii.

“Mpango huu unalenga kuimarisha huduma na kupanua wigo wa upatikanaji wa huduma za afya za kinga. Kuanzia Zanzibar mwaka huu ni hatua muhimu katika kuhakikisha wananchi wanapata nafasi ya kuchunguza afya zao mapema na kuchukua hatua za kinga,” amesema Sandra.

Kambi hiyo ni sehemu ya mpango wa muda mrefu wa Vodacom Tanzania Foundation wa kutoa makambi ya afya bure, ambao umetekelezwa kwa miaka mitatu katika mikoa saba na wilaya 16 nchini Tanzania Bara. Mwaka huu, mpango umepanuliwa Zanzibar, huku wakazi wakihimizwa kushiriki kwa wingi.

Wakazi wa Zanzibar wanahimizwa kushiriki kambi hiyo ili kuweza kuchunguza afya zao, kupata elimu ya kinga na kuchukua hatua mapema dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza, hatua inayoweza kuokoa maisha na kupunguza gharama za matibabu kwa muda mrefu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *