Maelfu ya waumini na wafuasi wa Imam Mahdi (Mwenyezi Mungu Aharakishe Kudhihiri Kwake) wamekusanyika katika Msikiti mtukufu wa Jamkaran, mjini Qom, katika siku tukufu za mwezi wa Sha’ban, na kuugeuza eneo hilo kuwa ishara yenye nguvu ya imani, mshikamano, na matarajio yenye matumaini kwa mustakabali wa baadaye.
Mkusanyiko huo umeakisi kwa kina utambulisho wa Kimahdawi (Imam Mahdi-ATF-) uliokita mizizi katika jamii ya Iran, na unaonesha namna imani ya Kiislamu, matumaini ya pamoja, na misingi ya mapinduzi ya Kiislamu yanavyoendelea kuathiri na kuunda maisha ya umma nchini Iran.
Kwa mujibu wa taarifa za wasimamizi, tukio hilo lilikuwa mkusanyiko mkubwa zaidi wa Kimahdawi tangu ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, uliofanyika kuadhimisha siku ya 15 ya Mwezi waa Sha’ban maarufu kama Nisf Sha’ban ambayo ni siku ya kukumbuka kuzaliwa kwa Imam Mahdi (ATF).
Msikiti wa Jamkaran, ambao kwa muda mrefu umetambuliwa kama kitovu kikuu cha kiroho kwa wale wanaomsubiri Imam Mahdi, ambaye ni Mwokozi Aliyeahidiwa, uliendelea tena kuwa kitovu cha ibada na utiifu wa kitaifa.
Hujjat al-Islam Seyyed Ali-Akbar Ojaqnejad, msimamizi wa Msikiti mtukufu wa Jamkaran, alielezea Nisf Sha’ban kuwa ni:
“Ni sikukuu kuu ya matumaini, kungojea kwa uelewa, na mustakabali wenye mwangaza kwa wanadamu.”
Amesisitiza kuwa tukio hilo linakumbusha ahadi ya Mwenyezi Mungu kuhusu kuanzisha mfumo wa haki, usawa, na kuheshimiwa kwa utu wa binadamu.

Hujjat al-Islam Ojaqnejad amesema Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ni kielelezo cha “kungojea kwa vitendo” kwa Imam Mahdi (AS).
Amesema mapinduzi hayo yalichangia kwa kiasi kikubwa kufungua njia ya kutimia kwa ustaarabu mpya wa Kiislamu.
Msikiti wa Jamkaran, kama kitovu kikuu cha mkusanyiko wa wafuasi wa Mahdawi, kwa mara nyingine tena ulipokea umati mkubwa wa waumini katika maadhimisho ya Nisf Sha’ban.
Mkutano huo ulifanyika chini ya kaulimbiu: “Mahdi, Roho ya Iran.”
Tukio hilo halikuwa tu mkusanyiko wa kidini, bali pia lilikuwa ni onyesho la nguvu laini (soft power) ya Iran inayotokana na imani, likisisitiza uhusiano wa karibu kati ya itikadi ya Mahdawi, utambulisho wa kitaifa, na maadili ya kimapinduzi.
Kwa mujibu wa waandaaji, mkutano huo unatuma ujumbe ulio wazi kwa ulimwengu wa Kiislamu na mataifa yote yanayodhulumiwa duniani: ujumbe wa kungojea kwa uelewa, upinzani dhidi ya dhuluma, imani thabiti, na matumaini ya mustakabali wa haki chini ya uongozi wa Imam Mahdi (AS).
Mkusanyiko wa Jamkaran ulithibitisha tena kwamba dhana ya kungojea kudhihiri Imam Mahdi (AS) nchini Iran si ya kusubiri kimya kimya, bali ni nguvu hai inayochochewa na imani, inayounda mshikamano wa kijamii, utambulisho wa kitaifa, na maono ya haki ya dunia nzima.