Jopo hilo linalowajumuisha waliokuwa marais walikutana na Rais wa Uganda, Yoweri Museveni na kumtaka ajihusishe moja kwa moja katika juhudi hizo kwani pande zote katika mzozo huo zinamtaja kuwa miongoni mwa watu wenye ushawishi kufikia suluhu la kudumu
Museveni amekubali kufanya hivyo akisema ifahamike kuwa hakuna upande unaotaka kuigawanya nchi ya Kongo, bali raia wa nchi hiyo kuishi kwa amani na maridhiano.
Jopo hilo linalohusika na mchakato wa upatanishi linalowajumuisha marais wa zamani akiwemo Rais wa Togo Faure Gnassingbé, Uhuru Kenyatta wa Kenya, Sahle-Work Zewde wa Ethiopia, Catherine Samba-Panza wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Olusegon Obasanjo wa Nigeria, na Mokgweetsi Eric Keabetswe Masisi wa Botswana.
Marais hao wamepewa jukumu hilo na Umoja wa Afrika kupatanisha pande zinazohusika katika mzozo wa mashariki mwa Kongo ikiwemo serikali ya nchi hiyo, wapiganaji wa M23 pamoja na Rwanda ambayo imedaiwa kuwaunga mkono wapiganaji hao, ingawa Rais Paul Kagame amekuwa akisisitiza kuwa kundi hilo lilianzisha harakati zake wakiwa Uganda.
Obasanjo apongeza juhudi zinazofanywa na mataifa ya nje
Obasanjo amepongeza juhudi zinazofanywa na mataifa ya Marekani na Qatar katika kufikia suluhu kwa mzozo huo ambao umeshuhudia sehemu kadhaa za mashariki mwa Kongo zikidhibitiwa na waasi wa M23 Lakini ametoa angalizo kuwa Umoja wa Afrika na mataifa mengine jirani na DRC yanatakiwa kuhusika moja kwa moja katika kufikia suluhu la kudumu.
Kwa upande wake Gnassingbé ambaye ndiye kiongozi wa jopo hilo amemwomba Rais Museveni kuhusika kuwa moja katika juhudi hizo kwani baada ya wao kukutana na Rais Kagame, Rais wa Kongo Felix Tshisekedi na viongozi wa M23 na pia Burundi wamepata kuthibitishiwa kuwa anafahamu vyanzo vya mzozo huo na anaweza kuchangia pakubwa katika kufanikisha upatikanaji wa amani na uthabiti mashariki mwa DRC.
Uganda na Rwanda zimehusika moja kwa moja katika mizozo ya Kongo, tangu wakati walipomsaidia marehemu Laurent-Désiré Kabila kuingia madarakani pale alipoung’oa utawala wa Rais Mobutu Seseko.
