
Shirika la Mpango wa Chakula Duniani, WFP limesitisha shughuli zake katika baadhi ya maeneo ya kaskazini mwa Sudan Kusini baada ya msafara wake uliokuwa umebeba tani 1,500 za misaada ya kiutu kushambuliwa na kuporwa. Kulingana na WFP, msafara huo wa misaada muhimu ya chakula iliyokuwa ikisafirishwa kwa njia ya mto ilishambuliwa wiki iliyopita katika jimbo la Upper Nile, ambalo pia limeshuhudia ghasia kubwa mwaka uliopita.
Misaada hiyo pia iliyokuwa na bidhaa zisizo za chakula kutoka kwa washirika, iliporwa usiku kucha na hapakuwa na msaada wowote wa kiusalama kutoka kwa mamlaka za eneo hilo, licha ya kuhakikishiwa usalama.
Wiki iliyopita, WFP na Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka, MSF walilaani vizuizi vya serikali dhidi ya upatikanaji wa misaada ya kibinadamu katika jimbo la Jonglei.