
Katika taarifa ya WFP iliyotolewa leo huko Juba, mji mkuu wa Sudan Kusini, shirika hilo limelaani vikali uporaji wa tani 1,500 za msaada wa chakula na bidhaa nyingine muhimu zilizokuwa zikisafirishwa kwa njia ya mto huku likisisitiza kuwa huduma hizo zitasalia kusitishwa hadi hapo usalama wa wafanyakazi na washirika wake utakapohakikishwa na serikali ya Sudan Kusini ichukue hatua za haraka kurejesha bidhaa zilizoibiwa.
Hakuna usalama licha ya hakikisho
Mashambulizi hayo yametokea kati ya Januari 30 na Februari 1, yakihusisha kundi la vijana wenye silaha waliovamia mara kadhaa msafara wa boti 12 za WFP.
Licha ya hakikisho la usalama kutoka vyombo vya usalama na mamlaka husika, uporaji huo umefanyika usiku kucha bila hatua zozote kutoka vyombo vya usalama vya Kaunti ya Baliet.
WFP imetoa wito wa dharura kwa pande zote zinazohusika katika mzozo kuheshimu shughuli za kibinadamu ikisema, “mashambulizi dhidi ya wafanyakazi wa misaada ya kibinadamu hayakubaliki kamwe. Tunahimiza pande zote kulinda rasilimali ambazo ni muhimu kwa utoaji wa msaada.”
Tishio la njaa jimbo la Jonglei
Hali ya usalama imezidi kuwa mbaya pia huko jimboni Jonglei, ambapo miundombinu muhimu ya kibinadamu ikiwemo maghala na vituo vya afya vimeharibiwa kutokana na mapigano kati ya majeshi ya serikali na makundi ya upinzani. Matukio ya uharibifu yameripotiwa katika maeneo ya Akobo, Ayod, Nyirol, na Uror, jambo linalohatarisha uwezo wa WFP kuwafikia zaidi ya watu milioni 4.2 wenye uhitaji mkubwa.
“Vizuizi vyilivyopo njiani na mashambulizi ya kikatili yanatishia uwezo wa WFP kuwafikia zaidi ya wanawake, wanaume, na watoto milioni 4.2 walio katika mazingira magumu zaidi,” WFP imebainisha.
WFP kutohifadhi tena chakula Jonglei
Kutokana na ukosefu wa usalama, WFP imelazimika kusitisha mpango wake wa kuhifadhi tani 12,000 za chakula kabla ya msimu wa mvua kuanza katika Jimbo la Jonglei. Hatua hii inaleta hofu ya kuongezeka kwa njaa kwa familia zinazotegemea msaada wa dharura wa chakula, lishe, na fedha za kujikimu. Shirika hilo limeonya kuwa mashambulizi haya yanadhoofisha juhudi za kuokoa maisha katika nchi ambayo tayari inakabiliwa na athari mbaya za mapigano na mabadiliko ya tabianchi.
Kwa sasa, hatma ya mamilioni ya watu nchini humo inategemea utashi wa kisiasa na usalama wa miundombinu inayotumika kusambaza mahitaji hayo ya lazima.