Msumbiji imekuwa nchi ya kwanza kuanzisha upya chanjo ya kinga, huku kampeni kama hizo zikitarajiwa kufanyika pia Bangladesh na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC.
Msumbiji yaonesha njia katikati ya milipuko na mafuriko
Kwa mujibu wa mashirika hayo ya Umoja wa Mataifa Kampeni ya chanjo nchini Msumbiji inaanza wakati nchi hiyo ikiendelea kukabiliwa na mlipuko wa kipindupindu na athari za mafuriko makubwa yaliyowaathiri zaidi ya watu 700,000, kuharibu mifumo ya maji na usafi wa mazingira na kuongeza hatari ya magonjwa yatokanayo na maji machafu.
Chanjo ya kinga ilisitishwa duniani mwaka 2022, baada ya ongezeko kubwa la wagonjwa wa kipindupindu kulazimisha nchi nyingi kuelekeza chanjo zilizopo katika kukabiliana na milipuko ya dharura.
Kampeni ya UNICEF ya chanjo ya kipindupindu yazinduliwa katika kambi ya Al Hol nchini Syria.
WHO: kutoka kukabiliana na milipuko hadi kuzuia
“Uhaba wa chanjo duniani ulitulazimisha kuendelea kukabiliana na milipuko ya kipindupindu badala ya kuizuia,” amesema Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus. “Sasa tuko katika nafasi nzuri zaidi ya kuvunja mzunguko huo. Chanjo hizi zitaokoa maisha.”
Dkt. Tedros pia amewataka wazalishaji zaidi kuingia katika uzalishaji wa chanjo ya kipindupindu, akibainisha kuwa EUBiologics kwa sasa ndiyo kampuni pekee inayozalisha chanjo kwa kiwango kinachohitajika kwa kampeni za kitaifa.
Mamilioni ya dozi zatengwa kwa nchi zilizo hatarini zaidi
Jumla ya dozi milioni 20 zimetengwa kwa awamu ya kwanza ya kampeni za kinga, zikiwemo dozi milioni 3.6 zilizokwisha wasilishwa Msumbiji, dozi milioni 6.1 kwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, na dozi milioni 10.3 zinazopangwa kuwasilishwa Bangladesh.
Uzalishaji wa chanjo ya kipindupindu duniani umeongezeka karibu mara mbili, kutoka dozi milioni 35 mwaka 2022 hadi karibu dozi milioni 70 mwaka 2025, huku ufadhili ukitolewa na Gavi na ununuzi pamoja na usambazaji ukifanywa na UNICEF.
Gavi yaonya dhidi ya uzembe wa kimataifa
“Mahitaji makubwa ya chanjo ya kipindupindu katika miaka ya hivi karibuni yamekuwa ukumbusho mkubwa kwamba upatikanaji endelevu wa chanjo ni rasilimali ya umma ya dunia,” amesema Dkt. Sania Nishtar, Mkurugenzi Mtendaji wa Gavi. “Dunia haiwezi kumudu uzembe. Tunashukuru washirika wetu na wafadhili ambao msaada wao umewezesha kuanza tena kwa kampeni hizi muhimu za kinga.”
Kundi la wafanyakazi wa kampeni ya chanjo ya kipindupindu kinachoungwa mkono na UNICEF kinaongeza klorini kwenye maji yanayokusanywa kutoka kwenye hifadhi huko Goma, katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
UNICEF: kulinda watoto na kuzuia maambukizi
Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF, Catherine Russell, amesema ongezeko la chanjo litasaidia kuzuia dharura kubwa za kipindupindu kwa mara ya kwanza baada ya miaka mingi.
“Kuanza tena kwa chanjo ya kinga dhidi ya kipindupindu kutawalinda watoto na kusaidia kukomesha ugonjwa huu unaoambukiza kwa kasi,” amesema, akisisitiza kuwa chanjo lazima iende sambamba na upatikanaji bora wa maji salama, usafi wa mazingira na huduma za usafi binafsi.
Wagonjwa wa kipindupindu bado ni wengi licha ya hatua zilizopigwa
Kipindupindu bado ni tishio kubwa la afya ya umma duniani, kikienea kupitia chakula na maji yaliyochafuliwa na kusababisha kuhara na upungufu mkubwa wa maji mwilini, hali inayoweza kusababisha kifo endapo haitatibiwa haraka.
Zaidi ya wagonjwa 600,000 na karibu vifo 7,600 viliripotiwa kwa WHO kutoka nchi 33 mwaka jana, ingawa takwimu hizi zinaaminika kuwa chini ya hali halisi. Ingawa chanjo ni nyenzo muhimu, WHO na washirika wake wanasisitiza kuwa uwekezaji wa muda mrefu katika maji salama, usafi wa mazingira, ufuatiliaji wa magonjwa na ushirikishwaji wa jamii ni muhimu ili kukomesha kipindupindu kabisa.