WHO yaomba dola bil.1 za kukabiliana na majanga ya kiafyaWHO yaomba dola bil.1 za kukabiliana na majanga ya kiafya

WHO imeathirika kwa kiasi kikubwa kutokana na kupunguzwa kwa misaada ya kigeni kutoka nchi tajiri, na imepunguza kwa kiasi kikubwa ombi lake la dharura ikilinganishwa na miaka ya hivi karibuni. Shirika la Afya Ulimwenguni limesema kiasi hicho cha pesa ni cha chini sana ikilinganishwa na miaka ya hivi karibuni.

Mkuu wa idara ya dharura za afya wa WHO, Chikwe Ihekweazu, amewaambia waandishi wa habari mjini Geneva kuwa, licha ya kufanya maamuzi magumu sana, shirika hilo lina wasiwasi mkubwa kuhusu mahitaji makubwa yaliyopo na jinsi litakavyoyashughulikia.

”Leo, WHO inaomba dola bilioni moja ili kuendeleza huduma muhimu za afya katika hali hii mbaya ya dharura duniani mwaka 2026. Fedha hizi zitasaidia kushughulikia huduma za afya katika nchi 36 zenye uhitaji wa haraka, ikiwemo Ukanda wa Gaza Mashariki ya Kati, Sudan, Ukraine, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Haiti na Myanmar. Tuna wasiwasi mkubwa kuhusu mahitaji makubwa yaliyopo na jinsi tutakavyoyashughulikia duniani kote.”

Haiti Port-au-Prince 2025 | Watu wanaishi katika mazingira magumu katika maeneo yaliyogubikwa na mafuriko.
Watu wanaishi katika maeneo yaliyofurika katika mji wa Port-au-Prince, Haiti, wakati mvua kubwa zilizosababishwa na Kimbunga Melissa ikianza kuliathiri eneo hilo.Picha: Guerinault Louis/Anadolu/picture alliance

Karibu watu robo bilioni wanakabiliwa na mizozo ya kiutu

Kwa mujibu wa Ihekweazu, karibu watu robo bilioni wanaishi katika migogoro ya kibinadamu inayowanyima ulinzi wa msingi kabisa, kama vile usalama, makaazi na upatikanaji wa huduma za afya. Katika mazingira haya, mahitaji ya afya yanaongezeka kutokana na majeraha, milipuko ya magonjwa, utapiamlo au magonjwa sugu yasiyotibiwa.

Marekani ambayo kwa jadi imekuwa mfadhili mkubwa zaidi wa shirika hilo, imepunguza kwa kiasi kikubwa matumizi ya misaada ya kigeni chini ya Rais Donald Trump, ambaye siku yake ya kwanza baada ya kurejea madarakani Januari 2025 aliwasilisha taarifa kwa WHO kuhusu nchi yake kujiondoa kwenye shirika hilo.

Mwaka jana, WHO iliomba dola bilioni 1.5 lakini Ihekweazu alisema ni dola milioni 900 pekee zilizopatikana. Amesema WHO inabadilisha mkakati wake kwa kuwezesha washirika wa ndani 1,500 kufanya kazi zaidi kwenye maeneo yenye mizozo ya kiafya katika maeneo husika

Hospitali katika Ukanda wa Gaza zaelemewa

To view this video please enable JavaScript, and consider upgrading to a web browser that supports HTML5 video

Ujerumani ilikuwa moja ya wafadhili wakubwa 2025

Wafadhili wakuu wa dharura mwaka jana walikuwa Umoja wa Ulaya, Ujerumani, Japan, Italia na Uingereza. Mwaka huo, WHO ilishughulikia dharura 50 za kiafya katika nchi 82, ikiwafikia zaidi ya watu milioni 30 kwa huduma muhimu. Hata hivyo, kupunguzwa kwa ufadhili wa kimataifa kulisababisha vituo 6,700 vya afya katika mazingira 22 ya kibinadamu kufungwa au kupunguza huduma, hali iliyowanyima watu milioni 53 huduma za afya.

Maeneo yenye hali ya dharura yaliyopewa kipaumbele kwa mwaka 2026 pia yanaijumuisha Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo Myanmar, Somalia, Sudan Kusini, Syria, Ukraine na Yemen, pamoja na milipuko inayoendelea ya kipindupindu na ugonjwa wa Mpox.

Ihekweazu amesema iwapo ufadhili hautapatikana, hali hiyo bila shaka itaiacha dunia katika hatari zaidi ya milipuko na majanga ya kiafya, kwa kuwa changamoto hizi haziwezi kutoweka bila mshikamano wa kimataifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *