Afisa mwandamizi wa Ukraine anasema mazungumzo ya amani ya ngazi ya juu na nchi za Urusi na Marekani ya Februari 4, yalikuwa “ya kweli na yenye tija.”
Rustem Umerov, katibu wa Baraza la Usalama na Ulinzi la Kitaifa la Ukraine, alitoa maoni hayo kwenye mtandao wa kijamii baada ya mazungumzo ya pande tatu huko Abu Dhabi, mji mkuu wa Umoja wa Falme za Kiarabu.
Ujumbe wa Ukraine pia ulimjumuisha Kyrylo Budanov, Mnadhimu Mkuu wa Rais Volodymyr Zelenskyy. Urusi ilimtuma Igor Kostyukov, mkuu wa huduma ya intelijensia ya kijeshi inayojulikana kama GRU, na maafisa wengine wa jeshi. Waliungana na mjumbe maalum wa Marekani Steve Witkoff.
Umerov alisema kwamba mkutano huo “uliangazia hatua madhubuti na suluhisho la kivitendo.”
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio aliwaambia wanahabari Februari 4 kwamba “orodha ya vitu vilivyo wazi” “imepunguzwa sana.” Lakini aliongeza, “Habari mbaya ni kwamba masuala yaliyobaki ndiyo magumu zaidi, na wakati huo huo vita vinaendelea.”
Afisa wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani alisema mazungumzo hayo ya amani yataendelea Februari 5. Swali muhimu ni kwa kiwango gani washiriki wanaweza kuimarisha majadiliano yao kuhusu suala la eneo na hakikisho la usalama kwa Ukraine.
Urusi inasema vikosi vya Ukraine lazima viondoke kutoka eneo la mashariki mwa Donbas ambalo Urusi kwa upande mmoja ilitangaza kuwa eneo lake ililolitwaa.