Manchester, England. Kocha wa Manchester City, Pep Guardiola, ameonyesha kutoridhishwa na kanuni za Kombe la Carabao zinazomzuia beki mpya wa timu hiyo, Marc Guehi, kucheza fainali dhidi ya Arsenal itakayofanyika Machi 22 katika Uwanja wa Wembley.

Guardiola amesema klabu hiyo imeanza taratibu za kuiandikia Barua Baraza la Ligi ya England (EFL) ili kuomba kanuni hizo zibadilishwe na kumruhusu Guehi, aliyeigharimu City Pauni milioni 20, kushiriki fainali hiyo.

Beki huyo wa kimataifa wa England amesajiliwa baada ya Manchester City kucheza mchezo wa kwanza wa nusu fainali, hali iliyomfanya azuiwe kushiriki mchezo wa marudiano na hivyo kukosa sifa za kucheza fainali kwa mujibu wa kanuni zilizopo.

Kanuni hizo zimerekebishwa msimu huu kuruhusu mchezaji kuichezea timu zaidi ya moja katika mashindano hayo, jambo lililomruhusu Antoine Semenyo kuichezea timu yake katika mechi zote mbili za nusu fainali dhidi ya Newcastle United. Hata hivyo, tofauti ya muda wa usajili imekuwa kikwazo kwa Guehi.

Beki wa Man City, Marc Guehi ambaye amejiunga na timu hiyo katika dirisha dogo la usajili akitokea Crystal Palace. Picha na Mtandao

“Natumaini Marc ataweza kucheza fainali. Unalipa pesa nyingi kumsajili mchezaji halafu unazuiwa kumtumia kwenye mchezo wa fainali, hilo silielewi. Ni fainali sasa, kwa nini asicheze? Tunalipa mshahara wake na ni mchezaji wetu halali.” amesema Guardiola.

Guardiola ameongeza kuwa tayari ameagiza uongozi wa klabu kuandika barua rasmi kwa EFL, ingawa hana matumaini makubwa ya mabadiliko kufanyika.

“Kubadili kanuni hapa England si rahisi, lakini tutajaribu,” amesema.

Katika hatua nyingine, Guardiola amesema nahodha Bernardo Silva ana mashaka makubwa ya kuichezea City katika mchezo wao wa Ligi Kuu dhidi ya Liverpool kutokana na hali ya majeraha.

Kocha wa Newcastle United, Eddie Howe. Picha na Mtandao

Wakati huo huo, kocha wa Newcastle United, Eddie Howe, ameonyesha hofu juu ya hali ya mchezaji wake Anthony Gordon aliyelazimika kutoka nje ya uwanja kutokana na maumivu ya nyama za paja.

“Ni jambo linalotia wasiwasi mkubwa,” amesema Howe baada ya timu yake kucheza mchezo wa sita mfululizo bila ushindi.

“Hakuna mapumziko. Tunapaswa kurejea kwenye ushindi haraka. Nimekerwa na kiwango chetu cha kipindi cha kwanza; hatukuwa imara wala makini kama tunavyojivunia kuwa.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *