Kocha wa timu ya soka ya Manchester City, Pep Guardiola, amesema mauaji ya watu wasio na hatia duniani kote yanamuathiri sana na amewahimiza walimwengu wasinyamazie kimya dhulma zinazofanywa.

Guardiola ametoa wito huo alipozungumza katika mkutano na waandishi wa habari kabla ya mechi ya nusu fainali ya Kombe la Carabao iliyofanyika kati ya timu yake na Newcastle United.

“Hatujawahi katika historia ya wanadamu kuwa na kila kitu waziwazi mbele ya macho yetu (kama hivi),” ameeleza kocha huyo wa Manchester City na kufafanua: “Mauaji ya kimbari huko Palestina, yaliyotokea Ukraine, Russia, Sudan – kila mahali. Hili ni tatizo letu kama wanadamu.”

Kocha huyo mwenye umri wa miaka 55 amesema, suala hilo limevuka mipaka ya siasa au kuegemea upande fulani, akisisitiza kwamba kulinda maisha ya mwanadamu lazima kutangulizwe kwanza.

“Si kuhusu Palestina pekee. Ni kuhusu kila piganio linaloweza kuufanya ubinadamu uwe na hali bora,” ameeleza Guardiola na kuendelea kubainisha: “watu wanaokimbia vita, wakiacha nchi zao, wakivuka Mediterania – usiulize kama ni sahihi au si sahihi (wanachofanya). Waokoeni. Wakati watu wanapokufa, inapasa uwasaidie”.

Huku akikosoa mauaji ya Renee Good na Alex Pretti yaliyofanywa na maafisa wa serikali kuu ya Marekani huko Minneapolis mwezi uliopita, Guardiola amesema matukio hayo yameonyesha kuwepo haja ya kupinga dhulma. “Tazama kilichotokea Marekani — Renee Good na Alex Pretti waliuawa,” amesema kocha huyo wa Man City, na kueleza bayana kwamba, vifo hivyo haviwezi kutetewa.

“Kama kitu ni kosa, nenda mahakamani, shtaki, pelekwa jela. Hiyo ndiyo jamii ya kisasa,” ameeleza nyota huyo wa soka wa zamani.

Guardiola amesema, inaumiza kushuhudia picha za raia wakiteseka licha ya maendeleo ya kisasa ya kiteknolojia na kijamii.

“Tunaweza kufika mwezini, tunaweza kufanya mambo ya ajabu, lakini tungalia tunauana. Ninapoona picha hizo, inaniumiza. Wakati maelfu ya watu wasio na hatia wanauawa, inaumiza. Daima nitasimama dhidi ya hayo. Unapoona akina baba, akina mama, watoto wakiharibiwa maisha yao kila siku, unawezaje kutohisi kitu? Mimi ninahisi,” amesisitiza kocha huyo wa Manchester City…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *