Hofu yatanda baada ya M23 kuulenga uwanja wa ndege KisanganiHofu yatanda baada ya M23 kuulenga uwanja wa ndege Kisangani

Kundi la waasi la AFC/M23 lilidai kuhusika na shambulio la droni Jumapili iliyopita katika Uwanja wa Ndege wa Bangoka huko Kisangani. Kulingana na mamlaka katika jimbo la Tshopo, droni nane pia zilikamatwa. Hata hivyo, hakuna majeruhi walioripotiwa na usafiri wa anga haukusitishwa.

Tukio hilo lilizusha hofu miongoni mwa raia ambao baadhi walilazimika kuyahama makaazi yao. Jean Etongo ni mkulima anayeishi karibu na uwanja huo wa ndege wa Bangoka huko Kisangani na anasema walihofia kutokea kwa vifo ikiwa wangeliangukiwa na droni, hivo wanakijiji walianza kuondoka kwa wingi usiku huo.

Tangu wakati huo, Etongo amekimbilia katikati mwa mji wa Kisangani, takriban kilomita 17 kutoka uwanja huo wa ndege ulioshambuliwa. Sasa anaishi katika jumba lililotelekezwa lisilo na milango wala madirisha. Kama Jean Etongo, bi Espérance pia alikimbia kijiji chake baada ya kusikia miripuko na hapa anaeleza.

Wanajeshi wa Rwanda wakipiga doria mitaa ya mji wa Kisangani tarehe 11 Juni 2000
Wanajeshi wa Rwanda wakipiga doria mitaa ya mji wa Kisangani uliokuwa karibu kuharibiwa kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, tarehe 11 Juni 2000 mara tu baada ya makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya majeshi ya Uganda na Rwanda.Picha: Emmanuel Goujon/dpa/picture alliance

“Askari hawakutaka tuondoke. Ni hofu yetu wenyewe iliyotufanya tuondoke, huku milio ya risasi ikiwatia wasiwasi watoto wetu. Droni ilipokaribia, tulisikia milio ya risasi, na wakati kulikuwa na mripuko mkubwa, hii ilimaanisha kuwa droni hiyo ilikuwa imedunguliwa na baadaye hali ya ukimya ikarejea.”

Kulingana na ujumbe rasmi uliotangazwa kwenye televisheni ya taifa, mamlaka za Kongo zilisema kuwa droni hizo zilizokuwa zimebeba silaha zilikusudiwa kusababisha vifo na uharibifu wa mali huku ikitoa wito kwa raia kutokuwa na hofu, kuwa watulivu na kutojali taarifa za uvumi. Gentil Sefu, makamu mwenyekiti wa shirika la kiraia la New Dynamics anasema Kisangani inachukuliwa kuwa ngome ya mwisho inayolengwa na waasi hao wa M23  huku akiitaka serikali ya Kongo kufanya juhudi zinazohitajika ili kupeleka vifaa vya kisasa vya kijeshi eneo hilo ikiwa ni pamoja na vifaa vya ulinzi wa anga, droni na ndege za kivita.

Jiji la Kimkakati

Kisangani ni mji wa tatu kwa ukubwa nchini Kongo baada ya Kinshasa na Lubumbashi. Pia ni mji wa kimkakati wa kiuchumi na kijeshi ambao serikali ya Kongo haitakiwi kuupoteza kama anavyoelezea Alphonse Maindo, profesa wa masuala ya siasa katika Chuo Kikuu cha Kisangani.

Viongozi wa kikanda wajadili amani ya DRC Uganda

To view this video please enable JavaScript, and consider upgrading to a web browser that supports HTML5 video

“Eneo hili ni njia panda ya kimkakati kati ya mashariki na magharibi. Ukiidhibiti Kisangani, unaweza kufika Kinshasa kwa urahisi kupitia mtoni. Kisangani pia ina rasilimali nyingi za asili kama mbao, madini ya dhahabu na almasi. Kijeshi, Kisangani imekuwa moja ya vituo muhimu vya jeshi la Kongo. Pia ni makao makuu ya eneo la tatu la ulinzi, na kwa hivyo, inaeleweka kwamba maadui wa Kongo wanaizingatia Kisangani kama shabaha kuu ya kulengwa.”

Mji wa Kisangani haujasahau makovu ya vita vya siku sita mnamo Juni mwaka 2000. katika mapigano kati ya majeshi ya Rwanda na Uganda. Hasa wakati huu kukishuhudiwa vitisho vipya, wakaazi wa mashariki mwa DRC wanatamani jambo moja kuufunga ukurasa wa migogoro na hatimaye kuishi kwa amani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *