Je, Afrika itanufaika na kupanda kwa bei za dhahabu?Je, Afrika itanufaika na kupanda kwa bei za dhahabu?

Mwaka 2025, thamani ya dhahabu iliongezeka kwa asilimia 65, ikivunja rekodi kufikia zaidi ya dola 5,580 za Marekani kwa wakia mmoja, sawa na gramu 31, kabla ya kushuka tena kidogo. Wataalamu wa masoko ya fedha wanasema ongezeko hili linatokana na kuongezeka kwa hali ya sintofahamu katika masoko ya kimataifa, sera zisizotabirika za Marekani, na hatari za kifedha zinazoendelea. Hali hii imewafanya wawekezaji kukimbilia dhahabu kama njia salama ya kuhifadhi thamani.

Kwa kuwa Afrika inachimba zaidi ya robo ya dhahabu yote duniani, ongezeko la bei limeonekana kama fursa ya kuongeza mapato ya kigeni na ya serikali. Burkina Faso, kwa mfano, ilifikia uzalishaji wa tani 94 mwaka 2025 — ongezeko la zaidi ya tani 30 kutoka mwaka uliotangulia.

Vipande vya Dhahabu
Vipande vya DhahabuPicha: Frank Hoermann/SvenSimon/picture alliance

Mtafiti wa Taasisi ya Mafunzo ya Usalama barani Afrika, Marvellous Ngundu, amesema bara la Afrika linaweza kufaidika kupitia mapato ya mauzo ya nje, kodi na ongezeko la fedha za kigeni. Lakini anatahadharisha kuwa faida hiyo itapatikana ikiwa mianya ya mapato na biashara haramu ya dhahabu itadhibitiwa.

Ghana, ambayo ni mchimbaji mkubwa zaidi wa dhahabu barani Afrika, serikali inapitia upya sheria za madini ili kupata sehemu kubwa zaidi ya mapato. Maafisa wanasema mikataba ya sasa, inayojulikana kama stability agreements, inanufaisha zaidi kampuni za kigeni. Hata hivyo, makampuni makubwa ya uchimbaji, kama Newmont na AngloGold Ashanti, yameeleza wasiwasi wao kuhusu mabadiliko hayo.

Hatua kama hizo pia zimechukuliwa katika nchi nyingine, zikiwemo Mali, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Tanzania, zimeimarisha sheria za madini ili kuongeza udhibiti wa serikali kwenye rasilimali muhimu kama dhahabu, cobalt na coltan. Licha ya hatua hizi, China na Urusi zimeongeza uwekezaji wao katika migodi ya Afrika, hasa katika ukanda wa Sahel.

Tuko tayari kuisaka dhahabu

To view this video please enable JavaScript, and consider upgrading to a web browser that supports HTML5 video

Hata hivyo, licha ya kuchimba dhahabu nyingi, Afrika inamiliki asilimia mbili pekee ya akiba ya dhahabu duniani. Kwa kulinganisha, Marekani ina zaidi ya tani elfu nane za akiba. Wachambuzi wanasema tatizo kubwa ni kuuza dhahabu ghafi nje ya bara, hali inayozinyima nchi za Afrika thamani ya ziada inayopatikana kupitia usafishaji na uhifadhi wa dhahabu kama akiba ya taifa.

Kupanda kwa bei ya dhahabu kumeongeza uchimbaji haramu, unaochochea migogoro na vurugu. Nchini Afrika Kusini, wachimbaji haramu wanaojulikana kama zama zama wamehusika katika mapigano makali. Kwenye maeneo yenye migogoro kama Sudan, migodi ya dhahabu imekuwa uwanja wa mapigano, huku vifo vya wachimbaji vikiripotiwa mara kwa mara.

Licha ya vita vya wenyewe kwa wenyewe, Sudan ilitangaza uchimbaji wa tani 70 za dhahabu mwaka 2025 — kiwango cha juu zaidi katika miaka mitano — ingawa wachambuzi wanasema sehemu kubwa ya dhahabu hiyo husafirishwa kwa njia za magendo.

Kwa ujumla, wachambuzi wanaona ongezeko la bei ya dhahabu kama upanga wenye makali mawili: fursa kubwa ya kiuchumi kwa Afrika, lakini pia changamoto inayohitaji usimamizi madhubuti ili faida isigeuke mzigo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *