
Kundi la waasi wa M23 limedai kuhusika na shambulizi la ndege zisizo na rubani lililolenga uwanja wa ndege muhimu katika jiji la Kisangani kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, kilomita mia kadhaa kutoka eneo la kawaida la operesheni za kundi hilo lenye silaha.
Serikali ya mkoa wa Tshopo, ambayo Kisangani ndio jiji kuu, ilisema Jumatatu kwamba ndege nane zisizo na rubani za adui ziliharibiwa kabla ya kufikia shabaha yao.
Shambulizi hilo liliashiria kuongezeka kwa mzozo mashariki mwa Kongo, kulingana na waangalizi, huku M23 ikiwa haijafanya mashambulizi hapo awali mbali na eneo lililo chini ya udhibiti wake.
Madai yalitolewa jana na kundi hilo linaloipinga serikali ya mjini Kinshasa na linaloungwa mkono na Rwanda lilikuja siku moja baada ya tangazo kwamba Umoja wa Mataifa utatuma ujumbe katika eneo hilo tete hivi karibuni kusaidia kutekeleza usitishaji mapigano.