Halijoto katika baadhi ya maeneo ya Japani ni za joto kiasi kwa wakati huu wa mwaka, na kuongeza hatari ya theluji kuanguka kutoka kwenye paa. Lakini hali ya hewa ya dhoruba inatabiriwa katika maeneo ya kaskazini kuanzia Februari 5 usiku.
Mamlaka ya Utabiri wa Hali ya Hewa ya Japani inatabiri kwamba halijoto mnamo Februari 5 itafikia viwango vya Machi katika eneo la Tohoku kaskazini mwa Japani, pamoja na mkoa wa Niigata na eneo la Hokuriku.
Kuongezeka kwa halijoto kunaweza kusababisha theluji kuteleza kutoka kwenye paa, kuanguka kwa michirizi ya barafu na maporomoko ya theluji.
Shinikizo dogo la hewa litakaribia mkoa wa kaskazini zaidi wa Hokkaido, huku likiongezeka kwa kasi. Theluji na mvua, pamoja na upepo mkali, vinatarajiwa kuanzia Februari 5 usiku kaskazini mwa Japani.
Maafisa wa hali ya hewa wanatabiri kwamba theluji itadondoka na kufikia kilele Februari 8, huku mirundikano ikifikia sentimita 70 huko Niigata wakati wa saa 24 hadi Februari 8 asubuhi, sentimita 50 huko Tohoku na sentimita 40 huko Hokkaido na eneo la Chugoku.
Hata maeneo yaliyo kando ya pwani ya Pasifiki, ambayo kwa kawaida hayapati theluji nyingi, yanaweza kuwa na theluji Februari 7 na 8.
Maafisa wanasema theluji nyingi inaweza pia kuathiri usafiri katika maeneo mengine. Wanatoa wito wa tahadhari dhidi ya maporomoko ya theluji, pamoja na kukatika kwa umeme ambako kunaweza kusababishwa na theluji kwenye nyaya za umeme.