Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imeawaahidi wakazi wa mtaa wa Msumi, Kata ya Mbezi wilayani Ubungo kupata huduma ya uhakika wa maji safi kuanzia mwishoni mwa miezi huu.
Kukamilika kwa mradi huo kunatarajiwa kuwanufaisha wakazi zaidi ya 47,000 wa mitaa ya Msumi A, Msumi B, Msumi C na maeneo jirani.
Katika siku za karibu DAWASA imekuwa ikilalamikiwa na baadhi ya wakazi wa maeneo ya Dar es Salaam ikiwemo wilaya ya Ubungo na mradi huo unatarajiwa kuondoa kero hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari, Msimamizi wa mradi huo, Mhandisi Azizi Namanga amesema wamekamilisha hatua ya kulaza bomba kubwa la maji kwa umbali wa kilomita 14 na sasa wameanza Ujenzi wa tenki la kuhifadhi lita 500,000 za maji.
“Tumepokea Shilingi Milioni 500 zilizoahidiwa na Waziri Jumaa Aweso na kazi zinaendelea kwa kasi huku malengo yetu ni kuanza kusambaza maji ifikapo Februari 22, 2026.” amesema Mhandisi Namanga.
Upatikanaji wa maji sio wa uhakika kwa wakazi wa maeneo ya wilaya ya Ubungo na baadhi ya maeneo ya Kinyerezi amekuwa ukisababisha kuongezeka kwa gharama za maisha kwa wananchi hali inayotarajiwa kubadilika pindi mradi huo utakapokamilika.
Mhariri @moseskwindi