Maseneta nchini Marekani wameonesha wasiwasi kuhusu sehemu za mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kuendelea kukaliwa na kundi la waasi wa M23. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa, hayo yamewasilishwa katika mkutano na Rais Felix Tshisekedi.
Maseneta hao pia wameelezea wasi wasi wao kutokana na mgogoro wa kibinadamu unaondelea mashariki mwa DRC, na kusema kuwa watu milioni 26 wanakabiliwa na uhaba wa chakula na kusema kuwa hali hiyo haivumiliki.
Kundi la M23 limekuwa kati kati ya mvutano huo mashariki mwa DR Congo.
Rwanda ikituhumiwa kuliunga mkono kundi hilo, kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa na mataifa ya Magharibi, kundi hilo linadhibiti sehemu kubwa ya eneo hilo, ikiwemo miji mikuu ya majimbo ya Goma na Bukavu, ambayo liliichukua mwanzoni mwa 2025.
Rwanda siku zote imekuwa ikikana tuhuma hizo.
Kauli ya Jim Risch, wa Republican kutoka Idaho, na Jeanne Shaheen, wa Democrat kutoka New Hampshire, mwenyekiti na mjumbe wa Kamati ya Mambo ya Nje, imekuja saa kadhaa baada ya Muungano wa Congo River Alliance, kundi la kisiasa la wapiganaji ambalo pia linajumuisha wapiganaji wa M23 lilikiri kujihusisha na shambulio la wiki iliyopita lililotokea Kisangani katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Bangoka kaskazini mashariki mwa DR Congo..